Mkuu wa wilaya Newala Alhaj. Mwangi Kundya imetaka jamii kuwaandalia wazee mazingira rafiki yatakayowawezesha kujikita katika shughuli za kiuchumi zitakazowasaidia kuwapunguzia kuwa na utegemezi na kulinda afya zao.
Ameyasema hayo mjini Newala wakati anafungua kikao cha siku mbili cha baraza la wazee la mkoa wa Mtwara kichofanyika katika ukumbi wa chuo cha uuguzi na ukunga Newala na kueleza kuwa kwa sasa wazee hawapewi kipaumbele cha kujikwamua kiuchumi.
“Imefika mahala hata wazee wameanza kudai mikopo ya wazee, fikra inayokuja haraka kwamba tutawafunga wazee wetu bure watashindwa kulipa, lakini hakuna ubishi hata kidogo wa umuhimu wa wazee kujikita katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali kama kilimo au biashara ili kupunguza ukali wa maisha ya utegemezi”.
Aidha Mkuu wa wilaya ameongeza kufafanua kuwa, wazee wanapojishughulisha katika kazi mbalimbali ni hatua muhimu kwao inayosaidia kuimarisha afya zao kwa kuwa zingine ni sehemu ya mazoezi ya mwili.
Kwa upande wake makamo mwenyekiti wa baraza hilo na mwenyekiti wa baraza la wazee manispaa ya Mtwara Mikindani Bi. Sesilia Herio amesema ili kwenda sawa na kaulimbiu yao ya “Uzee wa Kuchakaa Haukubaliki” wazee wanahitaji kufanyakazi.
“Nasisi wazee tupo kwenye kundi maalum lakini tunaachwa kwamba anae mtoto hii sii sawa, uzee umetofautiana, mtu ukiwa miaka 70 hadi 80 mwingine unakuwa na nguvu ya kufanyakitu wewe mwenyewe na ndio mana tunaomba mikopo”.
Hata hivyo afisa ustawi wa jamii kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mtwara Bi. Teresia Ngonyani ameisisitiza jamii kuwathamini, kuwaheshimu, kuwalinda na kuwatunza wazee na kuyafanyia kazi maoni yao “usije ukamuona mtu wa zamani, muhimu kuwasikiliza maana anaweza akakupa angalizo na lile angalizo likakusaidia kule unako elekea”.
Mabaraza ya wazee yapo kisheria chini ya sera ya taifa ya wazee ya mwaka 2003, kwa lengo la kuwa na sauti moja ya wazee, kusaidia katika kutoa maamuzi pamoja na ushauri utakaosaidia kulijenga taifa katika maadili mema na jamii kuzitambua tunu za taifa.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki miliki©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa