Halmashauri ya mji Newala imeanza kutekeleza kwa vitendo agizo la mkuu wa mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa la kuwaondoa wananchi walioshikilia maeneo bila kuyafanyia kazi katika miundombinu ya umwagiliaji ya Chikwedu Chipamanda na Lipeleng’enye.
Hayo yamebainishwa na Ofisa kilimo na umwagiliaji anayesimamia miundombinu hiyo Bw. Nelson Mtunga wakati wa kuanza zoezi la kimkakati la kusafisha mifereji na kuwatambua wanaomiliki maeneo kwenye skimu ya umwagiliaji ya Chikwedu Chipamanda lililoanza hii leo Jumatano 11/09/2019.
Bwana Mtunga amesema serikali kupitia wafadhili walishaweka miundombinu ya umwagiliaji katika skimu hizo na kutokana na changamoto ya wakulima wengi kutoyafanyia kazi maeneo yao, Mkuu wa Mkoa aliagiza mashamba yao wapewe vijana waliotayari kulima na kujiongezea kipato ili kulinda miundombinu hiyo na kufikiwa lengo kusidiwa la serikali la kuwanufaisha wananchi.
Mtunga alisema “kwa upande wetu kama halmashauri kwa kushirikia na watendaji wa vijiji tumeamua kuwatambua wamiliki kwa majina na ukubwa wa mashamba yao lakini jambo la muhimu ni hili ambalo tumelianza leo, kwanza kusafisha hii mifereji zoezi linalowahusu watu wote wenye maeneo na wasionao, tumepanga wale watakaoshindwa kushiriki tutayachukua maeneo yao na kuwamilikisha wengine kwa taratibu zote za kisheria, lakini vilevile wenye maeneo makubwa wanaoshidwa kuyamudu kuyafanyiakazi itabidi tuyapunguze na kuwapatia watu wengine”.
Katibu wa umoja wa wamwagiliaji wa skimu hiyo Bw. Juma Mnonji amesema amefurahishwa na hatua hiyo ya halmashauri, kwani bonde hilo ni muhimu kwa shughuli za uchumi wa mtu mmoja mmoja na jamii kwa umjula na katiba yao inaelekeza adhabu kwa wale wasioshiriki usafi, ambayo ni kulipa faini hadi shilingi laki moja (Tsh. 100,000/=).
Hatahivyo amesisitiza kuwa ili kufikia lengo, ni lazima kuwe na ushirikiano baina ya umoja huo na serikali kupitia halmashauri, isimamie zoezi hilo kwani uzoefu unaonyesha watu hawajitumi pasipo kuongozwa na kusimamiwa hasa na viongozi wa juu, huku akifafanua kuwa umoja wa mwagiliaji na wananchi wanaozunguka bonde hilo, wamekubaliana kufanya usafi kwa pamoja kila Jumatano na Jumamosi.
Baadhi ya wakulima na wasio wakulima walioshiriki zoezi hilo, wamesema skimu hiyo ni muhimu kwa kujiongezea kipato na kujikimu na maisha yao, hivyo wanaomba wale walioyatelekeza mashamba na wenye mashamba makubwa wangepungiziwa ukubwa au kunyang’anywa na kupatiwa vijana wenye nguvu ili wayaendeleze.
Skimu ya bonge la Chikwedu Chipamanda lipo Kijiji cha Chikwedu, Kata ya Mcholi 1, Tarafa ya Mkunya halmashauri ya mji Newala Mkoani Mtwara, na ina ukubwa wa hekta 1200 lakini halitumiki hata kwa kiasi cha nusu yake.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki miliki©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa