Afisa Usimamizi wa Fedha mkoa wa Mtwara Bi. Upendo Muze amewaomba watendaji wa Halmashauri ya Mji Newala kuwekeza kwenye mfumo mpya wa ukusanyaji wa mapato wa TAUSI na kuwaelimisha watumiaji ambao ni walipakodi juu ya faida za mfumo huo.
Ameyasema hayo kwenye semina elekezi ya matumizi ya mfumo wa TAUSI kwa wakuu wa idara na watendendaji wa Kata na Vijiji wa Halmashauri hiyo iliyofanyika Machi 5, 2023 kwenye ukumbi wa mikutano Halmashauri.
Bi. Muze ameeleza kuwa mfumo wa TAUSI utamuwezesha mlipa kodi na mkusanya mapato wa ngazi ya chini kutosumbuka kuomba namba ya malipo kwa kwenda ofisini badala yake umetengenezewa mazingira wezeshi ya mteja kujiihudumia mwenyewe popote alipo kwa kutumia mtandao wa mawasiliano.
“Manufaa ya mfumo mpya wa tausi kiukweli ni mfumo mzuri na nirahisi, na mfumo huu wa TAUSI kwa sasahivi unamuwezesha yule anaekusanya mapato kuomba namba ya malipo au control number bila kufika huku ofisni, yaani anaweza kujihudumia mwenyewe huko aliko ili mradi awe na network.” Alieleza Afisa usimamizi huyo.
Aidha Muze amesema utendaji kazi wa mfumo huo ni mzuri hivyo ameiomba Halmashauri ya mji Newala kuwekeza katika utoaji elimu ili kuwezesha matumizi sahihi ya mfumo huo wa ukusanyaji wa mapato kwa njia ya mtandao kupita mashine za ukusanyaji mapato kielektroniki (POS).
Nae Mtunza Hazina wa Halmashauri hiyo Bi. Costantina Shao anasema lengo la Serikali ni kuhakikisha mashine zote za kukusanyia mapato zinafanya kazi kwa kutumia mfumo wa TAUSI ambapo katika halmashauri yake mpaka mwezi Februari 2023 jumla ya POS 28 zimeshasajiliwa kwenye mfumo na lengo ni kusajili mashine 48 hadi kufikia mwezi Aprili 2023.
Hata hivyo Shao ameipongeza Serikali kwa kuleta mfumo wa TAUSI kuwa unakwenda kupunguza gharama mbalimbali za uendeshaji kama za uchapishaji wa risiti za malipo ambazo zilikua zitumia karatasi nyingi sambamba na kupunguza gharama kwa mlipa kodi na mkusanyaji wa mapato kwa kuwa huduma itatolewa mahali walipo pamoja na udhibiti wa upotevu wa mapato wakati wa ukusanyaji na ulipaji wa kodi.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki miliki©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa