Kaimu Mkuu wa idara ya elimu sekondari Halmashauri ya Mji Newala Mwl. Innocent Kerenge amewataka wazazi kuondoa vikwazo na viashiria vya mapito salama kwa wanafunzi kwa lengo la kusaidia upatikanaji wa elimu bora na salama.
Mwl. Kerenge amesema kuwa mpango wa shule salama unatekelezwa katika shule zote 16 za sekondari chini ya mradi wa Sequip na umekuwa na matokeo mazuri hivyo amewataka wazazi kuunga mkono mpango huo.
“Hadi leo tarehe 6 oktoba 2025 tunapoongea mpango huu unatakelezwa katika shule zetu zote hivyo rai yangu kwa wazazi ni kuhakikisha wanaondoa viashiria vya mapito salama, wanafunzi wengine wanapita kwenye vijiwe vya bodaboda, wavuta bangi, misitu hii inahatarisha usalama wao”
Mwalimu wa unasihi katika shule ya sekondari Nambunga Elfrida Kabengua amefafanua kuwa mpango huo umekua na matokeo mazuri kwa kuleta ushirikiano wa pamoja baina ya wanafunzi, walimu, na wazazi.
“Wanafunzi sasa wapo huru wanatoa mawazo yao, wanatoa dukuduku zao lakini pia wanafunzi sasa hivi hawashindi njaa tena na imewafanya wanafunzi wasiwe watoro kwa kuwa chakula kinapatikana shuleni”
Aidha Mwalimu mlezi wa klabu ya shule salama katika shule ya sekondari Mtangalanga Maftaha Seif ameisisitiza jamii kuwa na ushirikiano na walimu katika kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi.
Katibu wa klabu ya wanafunzi ya shule salama sekondari ya Mtangalanga Nuria Shazi ameeleza mpango huo umewasaidia kujenga ujasiri, kujiamini na kuwa wepesi wa kuelezea changamoto mbalimbali zinazozawakabili.
“Kwahiyo kupitia hii klabu imetusaidia sisi wasichana kujiamini pia kujieleza bila wasiwasi kuna tabia ya wasichana kuwa na aibu tunashindwa kueleza shida zetu ila kupitia hili dawati tunaweza kueleza changamoto zetu”
Ibrahimu Mustafa na Tariq Chigogo wameeleza kuwa mpango wa shule salama umerahisisha kutengeneza mawasiliano mazuri na walimu wa nasihi ambao wamewachagua kuwafikishia changamoto zao na kupatiwa ufumbuzi kwa urahisi.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki miliki©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa