Idara ya kilimo ya halmashauri ya mji Newala imewataka vijana kujitokeza kwenye kilimo cha umwagiliaji kwa kuwa halmashauri hiyo inalo eneo kubwa lenye miundombinu ya umwagiliaji na wao ndio nguvu kazi ya Taifa kuelekea uchumi wa kati wa viwanda.
Hayo yameelezwa leo Jumatano 04/09/2019 na Mkuu wa Idara ya Kilimo, Ushirika na Umwagiliaji Bw. Calistus Komba wakati anaelezea wajibu wao kwa vijana wanaojishughulisha na kilimo ambapo ameeleza kuwa jukumu lao kubwa ni kuwawezesha kwenye mafunzo ya kitaalam ya kilimo bora pamoja na kuwashauri kwenye masuala ya masoko.
Komba amewataka vijana kujitokeza kwa wingi kwenye kilimo kwa kuwa halamashauri hiyo inalo eneo kubwa lenye miundombinu bora ya umwagiliaji iliyowekwa na serikali kupitia wahisani, likiwamo bonde la Lipeleng’enye lililopo Kijiji cha Chihanga Kata ya Mkunya lina hekta 190 na bonde la Chikwedu Chipamanda lililopo Kata ya Mcholi 1 lina hekta 1200 ambayo hayatumiki ipasavyo kwa kukosa watu wa kilima.
Hata hivyo amesema halamashauri hiyo ina vikundi 12 vilivyotambuliwa, vinavyojishughulisha na kilimo lakini kikundi cha Uvumilivu kilichopo Kata ya Makote ni cha kuigwa kwa kuwa vijana wanazalisha mazao mengi ya mbogamboga na ufugaji wa samaki kwa nguvu zao na idara ya kilimo iliamua kuwaunga mkono kwa kuwapatia utaalamu wa kilimo cha kisasa ili wazalishe kwa tija.
Katika hatua nyingine amewataka vijana kutambua kilimo kinafaida na kwakuzingatia sera na mipango ya serikali kwenye kilimo, wigo wa soko la bidhaa za kilimo umezidi kutanuka, kwani licha ya mazao ya Korosho na Ufuta ambayo yapo kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani lakini mazao ya Muhogo na Mbaazi yamepatiwa wanunuzi wa uhakika kwa msimu wa mwaka 2019.
Kwa upande wao vijana wa kikundi cha Uvumilivu kinachojihusisha na shughuli za kilimo cha ustani wameishukuru halmasahauri ya mji Newala na serikali kwa ujumla kwa kuwaunga mkono katika shughuli zao za uzalishaji na kuahidi kuendelea kujiimarisha zaidi katika uzalishaji kwa kuwa wanalo eneo la kutosha.
Kikundi cha Uvumilivu, kipo Kijiji cha Makote Kata ya Mkote halmashauri ya mji Newala, kina wanachama tisa (9) na eneo la ekari sana (7), mpaka sasa wamelima Nyanya, Bamia, Chainizi, Mchicha, Kabeji, ufugaji samaki na wanendelea na ujenzi wa banda la kufugia kuku.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki miliki©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa