Idara ya kilimo halmashauri ya mji Newala, leo Alhamisi tarehe 24/10/2019 imekutana na mawakala wa uuzaji Mbolea waliopo ndani halmashauri hiyo, kwenye kikao cha pamoja cha kupeana uelewa wa agizo la serikali kuhusu bei mpya elekezi ya ununuzi na uuzaji wa mbolea ya kukuzia (UREA).
Akizungumza katika kikao hicho, kaimu mkuu wa idara hiyo Ndg. Nelson Mtunga, amesema Serikali kupitia wizara ya kilimo imeshatoa mwongozo wa bei ya mbolea kuanzia kwa wasambazaji, mawakala na mkulima kwa lengo la kumlinda wananchi na unyonyaji wa kuuziwa bidhaa hiyo gharama kwa kubwa isiyoendana na uzalishaji wake.
Mtunga amafafanua kuwa agizo hilo limetolewa kwa kuzingatia uzalishaji na faida ya mfanyabiashara pamoja na mkulima na tathmini hiyo imefanywa na Mamlaka ya udhibiti mbolea nchini (TFRA), kwa mamlaka waliyonayo na katika eneo la halmashauri ya mji Newala bei elekezi ya kuuza inatakiwa isizidi Tsh. 52,929/= kutokana na mawakala wake kuwa na mitaji midogo ya kuagiza mbolea chini ya tani kumi.
Aidha amefafanua kuwa, gharama za uuzaji na kununua zinatofautiana kutokana na kiasi kinachonunuliwa na umbali lakini hairuhusiwi kuuza juu ya bei elekezi na endapo kutakuwa na changamoto yoyote, mawakala wawasiliane na kamati ya pembejeo ya wilaya ili washauriane na kupata ufumbuzi wa pamoja na si mfanyabiashara kuamua mwenyewe.
Kwa upande wao mawakala walioudhuria kikao hicho, wameipongeza hatua hiyo ya serikali kuwa ni ya muhimu kwani inatengeneza ukaribu wa utendaji kazi na wamefurahishwa kuona maombi yao ya kuleta pembejeo mapema kwa mwaka huu yamesikilizwa hivyo wamesisitiza ushirikiano huo uimarike zaidi na pale zinapojitokeza changamoto zipatiwe ufumbuzi vizuri, ili kufikia malengo ya pamoja.
Baadhi ya mawakala hao Bw. Mkumba Bakaari na Azim Muhibu wameshauri kuwa, pamoja na uamuzi nzuri wa serikali wa kutoa mwongozo wa bei, lakini pia iingilie kati suala usafirishaji na kutoa mwongozo kwani ipo changamoto kubwa ya wasafirishaji kujipangia gharama wanazotaka wao bila kuangalia hali halisi ya biashara.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki milikiĀ©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa