Mkuu wa Mkoa Mtwara Kanali Ahmed Abbas, leo Jumamosi July 29/07/2023 amefanya ziara ya kukagua ujenzi wa shule mpya ya Miembesaba mradi wa Boost na ujenzi wa mabweni mawili katika shule ya sekondari ya wasichana Nangwanda Halmashauri ya Mji Newala, nakuridhishwa nayo.
Kanali Abbas amesema, amefurahishwa zaidi na kasi ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa mabweni kutokana na kasi yake pamoja na usimamizi unaojionesha, huku akiomba mshikamano uendelee ili wanafunzi 285 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano mwezi wa nane waweze kuyatumia.
Hata hiyo amesema serikali ya mkoa Mtwara itaendelea kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi hiyo ili kujiridhisha na hatua zinazoendelea pamoja na kuona kama thamani ya mradi husika inazingatiwa na pale zitakapobainika kasoro hatua za kurekebisha zichukuliwe mapema.
“Pale tutakapo baini kasoro za matumizi ya fedha, tutachukua hatua za haraka kuhakikisha kasoro hizo hazijirudii kwenye miradi mingine au kwenye mradi kama huu unao endelea”. Alifafanua Mkuu wa Mkoa.
Aidha Mkuu wa mkoa amesissitiza ukamilishaji wa miradi hiyo ifikapo Agosti 15, kwani serikali imeshatoa fedha zote hivyo usimamizi uongezwe iweze kukamilika kwa wakati na matarajio ya wananchi na walengwa wa miradi hiyo wanufaike nayo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya Newala Alhaj. Mwangi Rajabu Kundya, amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa fedha alizotoa kutekeleza miradi hiyo inayokwenda kuchochea maendeleo ya wananchi wa Newala.
Akiongea Katibu wa Chama Cha Mapinduzi wilaya Newala Bi. Sophia Lipenye amesema chama kitaendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi yote inayotekelezwa na serikali huku akiwaagiza viongozi waliopewa dhamana ya usimamizi, kukamilisha miradi kama ilani inavyoelekeza.
Nae Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Newala Mhe. Yusuph Kateule, amempongeza Mkuu huyo wa mkoa kwa utaratibu wake wakufanya ufuatiliaji na kuelekeza mbinu za kukabiliana na changamoto zinazo bainika badala ya kutoa maagizo ya vitisho kwa wataalam.
Aprili 24, 2023 Halmashauri hiyo ilipokea shilingi milioni 331.6 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya Miembesaba kutoka mradi wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji kwa shule za Awali na Msingi (Boost) na Juni 30, 2023 ilipokea fedha zingine milioni 260 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili katika shule ya sekondari ya wasichana Nangwanda.
Katika ziara hiyo Mkuu wa mkoa Mtwara ameongozana na wakuu wa wilaya zote na wakurugenzi wa halmashauri zote za mkoa wa huo kwa ajili ya kujifunza mbinu na uzoefu toka kwa waliofanya vizuri wakati wa utekelezaji miradi.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki miliki©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa