Mkuu wa wilaya ya Newala Alhaj Mwangi Rajabu Kundya amewataka wanawake kushikamana na kuthubutu katika kushiriki na kuwania nafasi mbalimbali za uongozi serikalini kwa kufuata mfano wa viongozi waliopo madarakani akiwemo mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Ameyasema hayo kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani ngazi ya halmashauri ya Mji Newala katika kijiji cha Namiyonga Machi 04 2023, ambapo pia kwa kuzingatia kaulimbiu ya mwaka huu isemayo “ubunifu na mabadiliko ya teknolojia ni chachu katika kuleta usawa wa kijinsia” ambapo amewataka wanawake kutambua wanayo fursa ya kiutendaji sawa na wanaume kama ilivyoainishwa katika sheria ya utumishi wa umma ya mwaka 2007.
Hata hivyo Mhe. Mwangi amewasisitiza wanawake kua mikopo iliyotolewa na halmashauri ya mji inalenga kuwawezesha wanawake kiuchumi kuleta usawa wa kijinsia na kukidhi haja ya serikali kama ilivyoeleza katika sera ya kuwawezesha wanawake ya mwaka 2004 hivyo waitumie ipasavyo mikopo hiyo kukuza uchumi wa familia na taifa kwa ujumla.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Hamisi Namata amesema usawa wa kijinsia katika jamii unaanzia kwenye familia hivyo wanaume wawashirikishe wake zao katika maamuzi na mikakati ya maendeleo kwani mwanamke anamchango mkubwa katika kukuza pato la familia, na kwa kufanya hivyo kutapelekea usawa na kuondoa dhana ya mwanamke kuwa tegemezi.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli zilizofanywa na Halmashauri zinazowahusu wanawake Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Bi. Joice Israel amesema halmashauri imewezesha jamii kuunda vikundi vya vikoba na ujasiriamali 593 ambavyo asimilia 90 ya wanachama ni wanawake
“Aidha tumetoa elimu mashuleni ya kutokomeza ukatili wa kijinsia na aina za ukatili, pia tumefanikiwa kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake 178 kuanzia mwaka 2016 hadi mwaka machi 2023 vimenufaika” aliongeza Israel.
Nae mkuu wa mtandao wa polisi wanawake wilayani Newala( TPF-NET) Mkaguzi Msaidizi Tumaini Ngwanda amesisitiza suala la ulinzi shirikishi kwa jamii katika kuwatunza watoto wa kike na wanawake kutokana na vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ambao kwa sasa unaendelea kushamiri, hivyo jamii itumie mitandao ya simu kutoa taarifa kwenye mamlaka husika ili kukabiliana na hali hiyo.
Kwa upande wake Afisa elimu kwa umma kutoka taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Newala Fides Didas amewataka wanawake kuwa walinzi wa familia kwa kuwashauri waume zao kuwa waadilifu kazini kwa ajili ya usalama wa familia.
Hata hivyo baadhi ya wanawake walioshiriki maadhimisho hayo wameeleza kuwa wanawake wenyewe wantakiwa kujitoa na kushiriki katika shughuli mbalimmbali kama ujasiliamali, ajira rasmi na uongozi ili kujenga jamii yenye usawa na mshikamano kama lilivyo lengo la maadhisho haya.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki miliki©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa