Mkuu wa wilaya ya Newala Mhe. Mwangi Rajabu Kundya Jumatano Mei 18, 2022 amezindua zoezi la ugawaji wa hati miliki za kimila 1659 wilayani humo kwa wananchi wa vijiji vya Chilangala, Mitema na Mkulung’ulu.
Aidha Mhe. Kundya amewataka wanawake kuacha kuwa wanyonge na kuweka kipaumbele cha kurasimisha ardhi yao kwa kuwa hiyo ni hatua ya kumkwamua mwanamke kiuchumi na kukuza hali ya maisha ya mtu mmoja mmoja familia na Taifa zima kwa ujumla.
Mkuu wa wilaya huyo amewasisitiza wanawake kutobaki nyuma kwenye mambo yote yanayowakomboa na kuwanyanyua kiuchumi kwa kuwa mwanamke ndio njia sahihi ya kuikomboa jamii.
Kwa upande wake aliyekuwa Mratibu wa zoezi hilo la urasimishaji ardhi vijijini kutoka Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) Ndg. Antony Temu, amewaomba wananchi waliopokea hati hizo kwenda katika kujiletea maendeleo.
Hata hivyo Temu amefafanua kuwa, kazi ya MKURABITA ni kuwajengea uwezo wananchi kwa kuwainua kiuchumi kupitia rasilimali zao ambazo awali walikuwa wakizitumia pasipo kunufaika nazo ambapo mpaka sasa tayari wameshazifikia halmashauri 63 kote nchini.
Akizingumza kwa niaba ya wakurugenzi wa halmashauri za Wilaya na Mji Newala Ofisa Ardhi na Maliasili wa halmashauei ya wilaya Newala Bi. Magreti Likonda amewashukuru MKURABITA kwa uratibu na kuwawezesha wananchi ambao sasa jukumu limebaki kwao kuchukua hatua za kunufaika na hati hizo.
Naye Mratibu wa zoezi hilo halmashauri ya mji Newala Ofisa Ardhi Ndg. Salvatory Nginga amesema pamoja na mafanikio hayo yaliyofikiwa lakini zilikuwepo changamoto kadhaa ikiwemo kijiji kulikuwa hakijapimwa na hakikua na cheti cha ardhi ya kijiji hivyo mpango huu uliwezesha kutatua changamoto hiyo.
Baadhi ya wananchi waliopokea hati hizo Ndg. Jafo Nandonde na Rashid Machemba wameishukuru serikali na waratibu wa mradi kwa kuwa sasa ni kama wameshafunguliwa mlango kuelekea hatua za maendeleo kupitia rasilimali ardhi.
Katika mradi huu uliohusisha vijiji vitatu wilayani Newala, jumla ya hati miliki za kimila 913 zimetolewa halmashauri ya wilaya Newala, kijiji cha Chilangala hati 494 na kijiji cha Mitema hati 419 wakati halmashauri ya mji Newala ikuwa na kijiji kimoja cha Mkulung’ulu ambacho kimepata hati 746.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki miliki©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa