Jamii imeshauriwa kuweka kipaumbele katika kupambana na tatizo la utapiamlo kuanzia pale mama anapopata ujauzito kwani tatizo hilo bado lipo na athari zake ni kubwa na za muda mrefu.
Rai hiyo imetolewa na kaimu mganga mkuu wa halmashauri ya mji Newala Dkt. Athanase Emmanuel ambaye alikua katibu kwenye kikao cha kamati ya lishe cha robo ya nne 2018/2019, kilichofanyika jana 20/08/2018 ambapo amesema elimu zaidi inahitajika ili jamii iondokane na tatizo hilo.
Amesema matatizo kama ya udumavu wa akili wakati mwingine yanasababishwa na utapiamlo, kwa watoto wadogo kukosa matone ya vitamin A, chanjo na lishe bora hivyo ni wakati muafaka wa kuchukua hatua ili kutengeneza Taifa imara kuelekea uchumi wa viwanda.
Kwa upande wake Afisa elimu sekondari Mwl. Athuman Salum, akimuakilisha mwenyekiti wa kamati hiyo, amesisitiza na kushauri kuwa elimu ya utapiamlo kuwa ajenda ya kudumu kwenye vikao mbalimbali vya vijiji kata na kamati ya huduma za jamii ili watu wawe na uelewa ya kutosha juu ya tatizo hilo.
Hata hivyo ameitaka kamati hiyo kuhakikisha inazuia uuzaji wa chunvi zisizo na madini joto pamoja na kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua wafanyabiashara wanaouza bidhaa za chakula na viuatifilu katika maduka yao kwani si salama kwa watumiaji.
Naye Afisa lishe wa halmashauri hiyo Bw. Enos Kuzenza amesema lipo tatizo la watu kuendelea kutumia chunvi isiyo na madini joto hasa chunvi ya mawe kwa kuwa inaweza kusababisha matatizo ya kuharibika mimba kwa mama mjamzito au utindio wa ubongo kwa mtoto atakayezaliwa.
Kuzenza amesema kwenye robo hii ya nne, yapo mafanikio yaliyopatikana ikiwa pamoja na kutoa matone ya vitamin A kwa watoto 11,650 wenye umri wa miezi 6 na chini ya miaka 5 sawa na asilimia 96.7% na dawa za kutibu minyoo kwa watoto 10,102 wa miezi 12 na chini ya miaka 5 sawa na asilimia 97.4% ya malengo kusudiwa.
Aidha ameeleza kuwa wajazito 2414 kati ya 2868 waliohudhuria waliohudhuria kliniki walipatiwa dawa za kuongeza wekundu wa damu (FEFO), watoto 72 wamepatiwa matibabu ya utapiamlo mkali pamoja na vituo vyote 14 vya afya vimepatiwa chakula dawa na vifaa vya kuwatambua watoto wenye utapiamlo mkali.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki milikiĀ©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa