Serikali imesema kundi la wanawake na vijana likiwekewa mazingira mazuri ya uzalishaji katika shughuli za kilimo, litasaidia kufikia malengo ya taifa ya kuwa na kilimo endelevu cha kibiashara kinachokua kwa asilimia 30 hadi ifikapo mwaka 2030.
Hayo yameelezwa Agosti 01,2023 na Naibu waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Jumanne Sagini (Mb) wakati anafungua maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini katika viwanja vya Ngongo-Lindi ambapo amesema kaulimbiu ya mwaka huu imetambua umuhimu wa kundi hilo katika uzalishaji wa chakula kwenye kaya.
Aidha Mhe. Sagini ameeleza kuwa maonesho ya Nanenane yatumike kuchochea hamasa ya wananchi kuongeza kipato kupitia kilimo, ufugaji na uvuvi pamoja na kujifunza fursa za kuongeza ajira, upatikaji wa rasilimali mbalimbali, uzalishaji, uongezaji wa thamani na masoko.
Katika hatua nyingine amesema serikali haitavumilia machafuko yoyote yanayoweza kuondoa utulivu na amani iliyopo na kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama hususani jeshi la Polisi kudhibiti viashiria vya uvunjifu wa amani kwa haki na usawa, kufuatia migogoro ya wafugaji na wakulima iliyoanza kuibuka mkoani Lindi.
Mwenyekiti wa maonesho hayo Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bi. Zainab Telack amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia wakulima wa korosho pembejeo za bure pamoja na waafisa ugani pikipiki kwa ajili ya kuongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo na mifugo.
Amesama mikoa ya Lindi na Mtwara inajivunia kuwa na ardhi yenye rutuba, madini, gesi, misitu ya asili, mbuga za wanyama, bahari, maeneo ya historia pamoja na kuwa vinara wa uzalishaji wa mazao ya korosho na ufuta yanayoingiza fedha nyingi kwenye pato la taifa.
Aidha Mhe. Telack amewaalika wawekezaji katika mikoa hiyo na kueleza kuwa hilo ni eneo muhimu kwa uwekezaji katika sekta mbalimbali za kiuchumi na inatarajiwa kuwa uchumi wa taifa utabebwa na mikoa hiyo baada ya miaka michache.
Maonesho ya wakulima nanenane kanda ya kusini yanahusisha mikoa ya Lindi na Mtwara nakufanyikia katika viwanya vya Ngongo-Lindi mwaka huu yamebeba kaulimbiu isemayo “Wanawake na Vijana ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula”.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki miliki©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa