Serikali wilayani Newala imesema itaendelea kuunga mkono jitihada za kumkomboa mwanamke kwa kutekeleza sera ya wanawake na jinsia ya mwaka 2000 inayolenga uwepo wa usawa kwa wanawake na wanaume katika nyanja zote na kuondoa unyanyasaji kwa wanawake.
Hayo yameelezwa leo Ijumaa 08th March, 2019 na Katibu Tawala (DAS) wa wilaya ya Newala Bw. Danieli Zenda ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mwanamke duniani iliyofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Kata Kitangali wilayani humo.
Zenda amesema unyanyasaji wowote wa kijinsia kwa wanawake haukubaliki katika jamii ya watanzania “na kwamba mwanamke sasa anahitaji kupata elimu sawa na mwanaume anahitaji kupata ajira sawa na mwanaume na ipo dhana iliyojengeka eti labda mwanamke awezi kufanya kazi fulani kama bodaboda na kazi zingine kama hizo lakini hiyo si sawa kwani hata hapa yupo dereva bodaboda mwanamke” alisema.
Aidha kupitia kauli mbiu ya mwaka huu ya maadhimisho hayo inayosema “Badili fikra kufikia usawa wa kijinsia kwa maendeleo Endelevu” Katibu tawala huyo amewata wanaume kuwapa wanawake nafasi ya kuthubutu kufanyia kazi mawazo yao na hiyo ndio njia itakayosaidia kuwa na maendeleo ya pamoja.
Kwa upande wake Ofisa wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) wilayani Newala Bi. Fides Didas amesema wanawake wengi hasa waotafuta ajira na waliopo kazini wanakabiliwa na tatizo la rushwa ya ngono ambayo ni udhalilishaji na kikwazo cha maendeleo ya mwanamke hivyo pale vinapojitokeza ni vema karipotiwa.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii wa halmashauri ya wilaya ya Newala Bi. Christina Kambuga akisoma taarifa ya historia ya maadhimisho hayo amesema lengo lake ni kupinia haki mbalimbali za wanawake na tangu kuanzishwa kwake kumekuwa na mafanikio makubwa kama muamko wanawake kuwania nafasi mbalimbali za uongozi, kushiriki siasa, kupata elimu pamoja na kushiriki katika maamuzi.
Maadhisho hayo wilayani Newala yameadhimishwa kwa kufanya usafi, upandaji miti kwenye kituo cha Afya Kitangali, kuwatembelea na kuwafariji wagonjwa waliolazwa katika kituo hicho kwa kuwapatia zawadi za sabuni, maji na juisi, maandamano yaliyobeba ujumbe wa siku hiyo pamoja na vikundi mbalimbali vya muziki, kwaya, maigizo na ngoma.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki miliki©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa