Naibu waziri wa Kilimo Mhe. Omary Mgumba amewataka wakulima wa mikoa ya Lindi na Mtwara kutumia fursa ya udongo wenye rutuba kulima mazao mchanganyiko ili kuongeza kipato kwa kuwa serikali imeshaweka mazingira mazuri ya soko la uhakika kwa bidhaa za mazao.
Mhe. Mgumba ameyasema hayo jana 08/08/2019 wakati anawahutubia wananchi na wakulima waliohudhuria kwenye kilele cha maonesho ya sikukuu ya wakulima Nanenane kanda ya kusini yaliyofanyika katika viwanja vya Ngongo mkoani Lindi ambapo amesema ardhi ya mikoa hiyo inafaa kwa kilimo cha mazao mengi hivyo ni wakati wakuacha kutegemea zao moja.
Aidha ameeleza kuwa serikali tayari imeshatafuka soko la uhakika kwa mazao ya ufuta, mbaazi na korosho hivyo ni suala la mkulima kuongeza juhudi kwenye uzalishaji, huku akitoa uhakika wa ununuzi wa zao la korosho kwa msimu wa 2019/20120 kwani zilizopo maghalani zote zimepata mnunuzi na muda mfupi zitaondolewa kwenye maghala yote nchini.
Sambamba na hilo amesema kauli mbiu ya mwaka huu isemayo “Kilimo, Mifugo na Uvuvi Kwa Ukuaji Wa Uchumi wa Nchi” imezingatia mchango wa sekta ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo nchini, kwa pamoja vinachangia asilimia 65% ya malighafi za viwandani nchini, asilimia 75 ya ajira, asilimia 35 pato la Taifa na asilimia 30 fedha za kigeni hivyo huu ndio muhimili muhimu wa kufikia maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake mjumbe wa kamati ya kudumu ya mbunge ya Kilimo, Mifugo na Maji mbunge wa Namtumbo Mhe. Edwin Ngonyani akimwakilisha mwenyekiti wa kamati hiyo amesema kamati inaitaka wizara kupitia idara ya masoko kuongeza jitihata za kutafuta masoko ya mazao ya wakulima badala ya kuitegemea wizara ya viwanda na biashara pamoja na masoko ya walioanzisha viwanda vidogo vidogo.
Aidha katika utangulizi wa ujumbe wa wizara ya kilimo kupitia kwa mwakilishi wa katibu mkuu, amewataka wakulima kuzingatia mashariti ya matumizi sahihi ya viwatilifu kwa kuwatumia wataalam wa kilimo kwa kuwa lengo la serikali ni kuuza bidhaa za kilimo nje ya nchi hivyo ni lazima uzalishaji ukafanyika kwenye viwango bora vinavyohitajika.
Akizungumza na wananchi walioudhuria kilele cha sherehe hizo, Mke wa Rais mstaafu wa awamu ya nne (Mb) Mama Salma Kikwete amewataka wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara kutumia maonesho hayo kama chachu ya kuongeza uzalishaji na hatimae kufikia maendeleo kwa kuzingatia sera ya Taifa ya kuelekea uchumi wa kati wa viwanda kutokana na rasilimali zilizopo ndani ya mikoa hiyo.
Sikukuuu ya wakulima nchini huadhimishwa kila mwaka tarehe 08/08 sambamba na shamrashamra za maonesho ya wakulima na wafanyabiashara yanayofanyika kwenye kanda mbalimbali na kubeba kauli mbiu ya kitaifa ambapo kwa mwaka huu kauli mbiu inasema “Kilimo, Mifugo na Uvuvi Kwa Ukuaji Wa Uchumi wa Nchi.”
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki miliki©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa