Shirika la Viwango vya Ubora wa Bidhaa Nchini (TBS) makao makuu kwa kushirikiana na Shirika la viwanda vidogo vidogo (SIDO) mkoani Mtwara leo Alhamisi Mei 15, 2020 wametoa mafunzo ya kuzalisha bidhaa zenye viwango vya ubora kwa viwanda vinne vya ujasiriamali vinavyozalisha bidhaa halmashauri ya mji Newala.
Afisa mwezeshaji kutoka shirika hilo Bi. Dina Lwendo, akizungumza kwenye viwanda tofauti alivyotembea mjini Newala, amesema serikali baada ya kubaini kuwa bidhaa nyingi za wajasiriamali wadogo hazina nembo za ubora, imeagiza bidhaa zote zinazozalishwa nchini zikidhi viwango vya ubora na kuwa nembo, hivyo TBS imeamua kushuka chini kutoa uelewa kwa wazalishaji wadogo ambao wengi wao wameonekana kutokuwa na elimu ya kutosha.
Hata hivyo Bi. Lwendo amekiri kuwa bidhaa nyingi za wajasiriamali wadogo zinakosa soko la nje na hilo linadhihirika kwenye maonyesho mbalimbali ya biashara, kutokana na kutokuwa na nembo ya ubora na ndio maana TBS imeamua kutoa elimu kuanzia kwenye hatua za awali za uzalishaji ili kulinda ubora wa bidhaa tangu kiwandani na sio kupima maabara bidhaa zinazoingia sokoni pekee.
Aidha amesema ni matumaini yao kama wajasiriamali watapata elimu vizuri kwa kushirikiana na wataalamu mbalimbali chini ya SIDO na halmashauri matokeo yatakua makubwa kwani bidhaa nyingi zinao ubora wa kutosha tatizo lililopo ni kuwa zinakuwa hazijathibitishwa na hilo ndilo wanalolifanyia kazi.
Kwa upande wake Afisa mwezeshaji kutoka SIDO Mtwara Bw. Kasto Tamba amewataka wajasiriamali kuipokea fursa hiyo kwa mikono miwili kwa kuwa serikali imewajali kwani imewaunganisha SIDO na TBS kufanya kazi kwa pamoja, kurahisisha uhakikia wa bidhaa, majengo ya viwanda pamoja na hatua za uzalishaji ili kuondoa mlolongo wa zoeli hilo.
Hata hiyo amesema ipo faida kubwa kwa watakaokidhi vigezo vya kupatiwa nembo ya ubora kwa kuwa serikali imetoa muda wa miaka mitatu ya awali ya uzalishaji bidhaa kutumia nembo hiyo bila malipo yoyote na malipo hayo yatafanywa na wizara ya viwanda na biashara kwa lengo la kukusaidia kuimarisha mtaji wa biashara yako.
Naye msimamizi wa vikundi vya wajasiriamali halmashauri ya mji Newala Afisa Maendeleo ya Jamii wa halmashauri hiyo Bi. Frola Barakana ameishukuru serikali kwa kuwajali wajasiriamali wadogo kwani hiyo ndio njia pekee ya kuwakomboa na kuwaimarishia mitaji yao kwa kuwa changamoto ya ubora imeyumbisha soko la bidhaa nyingi za vikundi vya wajasiriamali.
Viwanda vya wajasiriamali vilivyotembelewa vimeishukuru serikali kupitia SIDO na TBS kwa kuwaona na kuwafikia kwenye maeneo yao hiyo inaonyesha nia ya dhati ya serikali kutaka kuwakwamua kiuchumi na wao wanaenda kuyafanyia kazi maelekezo waliyopatiwa kwa kuwa nia yao ni kuwa wazalishaji wakubwa na wafanikiwe kuuza bidhaa zao nje nchi.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki milikiĀ©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa