Halmashauri ya Mji Newala kupitia idara ya ustawi wa jamii imeanzisha kampeni ya kutoa elimu ya kutambua vitendo vya ukatili kwa wanafunzi waliopo shuleni wenye lengo la kupunguza vitendo hivyo na kujenga ustawi wa watoto.
Akizungumza leo 14 Julai 2022 viwanja vya shule ya msingi Karume mjini Newala baada ya kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule mbalimbali, Afisa Ustawi wa Halmashauri hiyo Bi. Melania Ng’itu amesema hatua hiyo inalenga kutekeleza sera ya serikali ya kupambana na ukatili kwa watoto hivyo ni wakati muafaka kwao kuwajengea uelewa waweze kuondokana na athari za vitendo hivyo.
Ng’itu amesema kutokana na maelezo ya watoto wenyewe inaonyesha kuwa katika mazingira ya shule na nyumbani wanatendewa vitendo vya ukatili huku baadhi yao wakiwa wanavitambua na hawajui njia za kupata msaada na wengine hawana uelewa kabisa jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa mtoto na kuitaka jamii kubadilisha mtazamo kuhusu malezi ya mtoto.
Kwa upande wake mwalimu wa michezo kwa shule za msingi wa Halmashauri hiyo Mwl. Zabron Mpini amepongeza hatua hiyo ya ustawi wa jamii na kueleza kuwa matendo ya ukatili kwa watoto yanaongezeka katika jamii na athari zake ni kubwa kwa afya ya mwili na akili pamoja hatma ya maisha ya baadae ya mtoto kwa kuwa hayasahauliki kirahisi.
Aidha amewaomba wazazi kuwa waangalizi na walezi bora kwa kuwa vitendo hivyo huanzia kwenye ngazi ya familia na yanapomkuta wanafunzi yanamuondolea uelekeo katika masomo na hata michezo kwa kuumizwa ndani ya akili na kama matendo hayo hayatasemwa ni kuwaangamiza.
Shania Shabani na Exiwanda Mnamwa wanafunzi wa darasa la saba kutoka shule ya msingi Nachituro wamesema wamepata uelewa juu ya ukatili na hatua wanazoweza kuzichukua pale watakapo kutana na matukio ya aina hiyo kwa kuwa mwanzo hawakujua wapi wanaweza kupata msaada pindi matukio ya unyanyasaji yakiwakuta.
Sambamba na mafunzo hayo ustawi wa jamii imetoa zawadi ya taulo za kike na sabuni za kufulia kwa wanafunzi hao walio kwenye kambi ya michezo.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki miliki©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa