Maafisa watendaji wa kata na vijiji wa halmashauri ya Mji Newala mkoani Mtwara wametakiwa kutekeleza wajibu wao wa ukusanyaji mapato ya halmashauri yaliyopo kisheria bila woga.
Agizo hilo limetolewa jana January 30, 2019 kwenye mkutano wa robo ya pili 2018/2019, wa baraza la Madiwani na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Mheshimiwa Saambili Mohamed ambapo amesema watendaji wanapaswa kuvitambua vyanzo vyote ya mapato kwenye maeneo yao na kuvitoza ushuru.
Aidha Mhe. Saambili amewataka waheshimiwa madiwani kutowawekea vikwazo watendaji hao wakiwa kwenye utekezaji wa majukumu yao kwani jambo hilio litapunguza mapato ya halmashauri ambayo kwa sasa ni madogo kutokana na vyanzo vingi kuchukuliwa na serikali kuu.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa niaba ya Mwenyekiti, Makamo Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Mhe. Othuman Bilali, amesema miradi yenye jumla ya zaidi ya shilingi bilioni nne imeanza kutekelezwa na tayari halmashauri imshapokea zaidi ya shilingi bilioni mbili kutoka serikali kuu na zaidi ya shilingi bilioni moja zimeshatumika katika kutekeleza miradi hiyo.
Akiongea kwenye mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Aziza Mangosongo, ameipongeza halmashauri hiyo kwa kufanya vizuri kwenye matokeo ya darasa la saba (7) 2018, kwa kukamata nafasi ya kwanza kimkoa na kwenye mbio za mwenge mwaka 2018, kuwa ya kwanza (1) kimkoa, ya nne (4) kikanda na ya sita (6) kitaifa na kueleza kuwa hayo ni matunda ya usimamizi nzuri wa fedha za miradi ya maendeleo.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya amewataka waheshimiwa madiwani kuwa na taarifa za wakulima wa korosho waliolipwa fedha zao katika maeneo yao, ili kuondokana na dhana potofu kuwa wakulima hawajalipwa kabisa fedha kwani hadi sasa wakuliwa wenye kilo chini ya 1500, wameshalipwa kiasi cha bilioni 47 kati ya bilioni 61 wanazostahili kulipwa wakulima wote wilayani hapa.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Newala ndugu Jabir Mtanda, amesema wao kama chama kinachosimamia utekelezaji wa ilani wameridhishwa na utendaji wa mkurugenzi wa halmashauri hiyo na wataalamu wake, hivyo ni vyema kuongeza mshikamano ili wananchi wapate maendeleo kusudiwa kwa urahisi.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki milikiĀ©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa