Wananchi wa mkoa wa Mtwara wametakiwa kutambua kuwa zao la muhogo ndio zao mbadala la chakula na biashara ikiwa wataliendeleza kwa kutumia mbinu na mbegu bora za kisasa.
Hayo yameelezwa Jumanne June 07, 2022 na Katibu Tawala (RAS) wa Mkoa huo Bw. Abdallah Malela katika mkutano wa wakujadili mbinu za kukuza uzalishaji na kuongeza tija kwenye zao la muhogo wilayani Newala, ulioandaliwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Newala kwa kushirikiana na mashirika pamoja na wadau wa zao hilo.
Bw. Malela amesema zao la muhogo ni muhimu kwa kuwa linafaa kwa chakula na biashara hivyo ni wakati wa wakulima kulipa kipaumbele. “zamani unapanda tu muhogo unashambuliwa na maradhi unabaki kulia, lakini leo tuna wataalam tena taasisi za kimataifa zimeingilia kati kuhakikisha kwamba kule kufuta machozi kila mwaka kwa mkulima kuwe basi.” alifafanua.
Hata hivyo Katibu Tawala amempongeza Mkurugenzi kwa kuandaa mkutano huo na kueleza kuwa hatua hiyo, imetokana na mwitikio wa kikao cha mpango mkakati wa Mkoa wa kukuza zaidi uchumi na pato la mwananchi wa Mtwara kutoka kwenye zao la korosho hivyo ni hatua muhimu kwa wanamtwara.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Newala Bi. Shamim Mwariko amesema mkutano huo umelenga kujenga mkakati ya pamoja wa kuliendeleza zao la muhogo kwa tija na kuibua fursa za kibiashara na masoko kwa kuwa wananchi wa Newala wanalima zao hilo kwa miaka mingi lakini hawalioni kuwa ni la uchumi.
Aidha Mwariko ameeleza kuwa Halmshauri ya mji Newala na wilaya kwa ujumla inayo sababu sababu ya kubadilisha mitazamo ya vijana ili wazione fursa mbalimbali za kibiashara zinazotokana na kilimo zitakazopelekea kuongeza thamani ya shughuli za kilimo na mazao yenyewe.
Mwakilishi wa taasisi zilizoalikwa kuwajengea uwezo wakulima na vijana, kutoka Taasisi ya Kimataifa Inayoangalia Tafiti za Kilimo Ulimwenguni (IITA) Dkt. Kiddo Mtunda amesema dira yao ni kuona ulimwengu unaondokana njaa, umasikini pamoja na kuhakikisha mazingira yanatunzwa vizuri hivyo wapo tayari kushirikiana na Halmashauri na Mkoa kwa ujumla katika kufikia malengo ya kukuza pato kwa wananchi.
Mmoja wa wazalishaji wa mbegu za muhogo za kisasa Bw. Ahmadi Kadembe (Fresh ya shamba) ameishukuru halmashauri ya mji Newala na kuwashauri wakulima kufanya kilimo cha kisasa huku akifafanua kuwa kwa unapotumia mbegu bora faida inakuwa kubwa na baadhi ya mbegu hutoa hadi tani 23.6 kwa hekta moja tofauti na mbegu za asili ambazo haziwezi kutoa kiwango hicho cha mazao na zinashambuliwa kirahisi na magonjwa.
Katika mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Newala, Halmashauri ilishirikiana na Taasisi ya kimataifa ya inayoangalia tafiti za kilimo ulimwenguni (IITA), Taasisi ya utafiti wa mbegu (TARI) Naliendele, Taasisi ya usimamaizi wa mbegu bora za Muhogo (MEDA), Taasisi kwa kifedha NMB-Foundation, TCB, CRDB, Wazalishaji wa mbegu bora za muhogo, wasindikaji, wakulima na vijana.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki miliki©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa