Mbunge wa Jimbo la Newala Mjini Mhe. George Mkuchika ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Maalum amewataka wananchi wa Newala kujihusisha na kilimo cha mazao mchanganyiko na kuacha kutegemea zao la korosho pekee.
Mheshimiwa Mkuchika ameyasema hayo Ijumaa July 14, 2023 akiwa kwenye siku ya pili ya ziara yake ya kijimbo ya kuongea na wananchi kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya serikali pamoja na kutoa ufafanuzi wa changamoto zinawakabili.
Amesema ni muhimu wakulima kuchukua hatua hiyo mambo yanabadilika na hata kwa msimu uliopita zao la korosho halikufanya vizuri. “Wapiga kura wangu wa Newala tusitegemee kilimo cha korosho peke yake mwaka jana msimu ulikua mbaya kwa korosho hatujui ni hali ya hewa.. hatujui tu, sasa basi una shamba la mkorosho lima na mbaazi, lima na mahidi ya kula”. Alisisitiza Mbenge huyo.
Aidha Mhe. Mkuchika amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kwapatia wakulima wa korosho pembejeo za bure huku akiwahimiza wakulima hao kuongeza jitihada katika uzalishaji kwa kuwa serikali imedhamiria kuliongezea thamani zao hilo kwa kuacha kuuza korosho ghafi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Yusuph Kateule amewataka wananchi kuchangia ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kulipa ushuru na tozo halali zilizoidhinishwa kisheria kwa kuwa ndizo chachu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya halmashauri.
Mwenyekiti Kateule amefafanua kwa mwaka wa fedha uliopita 2022/2023 malengo ya ukusanyaji mapato ya ndani hayakufikiwa kutokana na kuyumba kwa zao la korosho, baadhi ya wakulima kuuza mazao yao nje ya halmashauri pamoja na wafanyabiashara hasa wadogo kukwepa kulipa ushuru.
“Ndugu zangu jambo hili linatukwamisha sana kutekelezea mipango yetu ya maendeleo, tunashindwa kukamilisha miradi hivyo tunapokwepa kulipa ushuru sisi wenyewe ndio tunaathirika, hakikisheni unauza katika utaratibu uliowekwa katika kijiji chako”. Alifafanua Mhe. Kateule
Afisa Mipango wa Halmashauri ya Mji Newala Bi. Sophia Makungu amewahimiza wananchi kujiandaa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya mwaka wa fedha 2023/2024 kwa sehemu ya mchango wa jamii hivyo vijiji vyenye miradi kupitia wananchi waanze kukusanya mchanga, kusafisha maeneo na maandalizi mengine yanayohitajika.
Hii ni siku ya pili ya ziara ya Mbunge wa Jimbo la Newala Mjini Mheshimiwa George Mkuchika ambayo atafanya mikutano, kukagua shughuli na miradi ya maendeleo katika kata zote 16 za jimbo hili ambapo leo ametembelea Kata ya Namiyonga na Kata ya Makote.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki miliki©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa