Wasimamizi wa Elimu wa Halmashauri ya Mji Newala wameshauriwa kuingia darasani kufundisha masomo mbalimbali kulingana na ujuzi walionao ili kuisaidia jamii sawa na taaluma yao ya ualimu na kuacha kukaa ofisini pekee.
Wito huo umetolewa leo Ijumaa Julai 15, 2022 na Mthibiti Mkuu wa ubora wa shule wa Halmshauri ya Mji Newala Mwl. Hamisi Mbinga katika kikao cha wasimamizi wa elimu ngazi ya halmashauri cha kujadili namna ya kutekeleza maazimio yaliyotolewa na wasimamizi wa elimu ngazi ya Taifa mkoani Tabora.
Mbinga ameeleza kuwa kuanzia ngazi ya shule mpaka wizara wasimamizi wote wa elimu ni walimu, nafasi zingine walizo nazo ni ziada na wakati wowote wanaweza kuondoka na kurudi kufundisha hivyo si vibaya kwao kuendeleza umahiri wa taaluma yao kwa kutenga muda wa kufundisha darasani.
Aidha Mbinga amesema moja ya azimio lililowekwa katika kikao cha Taifa ni kuondoa ziro kwa sekondari mkakati ambao Mkoa wa Mtwara tayari ulishauweka katika mpango wake wa kuinua elimu, hivyo wasimamizi wakiwa mstari wa mbele kuweka msisitizo na kujitoa kwa vitendo itakua ni rahisi azimio hilo kufikiwa.
Mthibiti huyo ameongeza kuwa suala la nidhamu ni jambo lingine la muhimu la kuwezesha kupata matokeo chanya kwa kuanzia waalimu wenyewe na kama walimu wakikaa vizuri katika fundisha na kuhakikisha wanafunzi wanajua kusoma, kuhesabu na kuandika (KKK) ambapo mkoa umeweka kipaumbele eneo hilo na linahitaji nguvu ya pamoja.
Katika hatua nyingine Mbinga amesema ofisi yake ilibaini maeneo ambayo walimu wana changamoto ya kufikia ufundishaji wa kkk wameshatoa mafunzo kwa walimu na sasa halmashauri imepata mradi wa Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA) mpango amabao unatarajia kutoa matokeo chanya ya ufundishaji na kuondoa tatizo la KKK ifikapo mwezi Novemba mwaka huu.
Akizungumza kwa niaba ya wasimamizi wa elimu Mkuu wa idara ya elimu sekondari wa Halmashauri hiyo Mwl. Athuman Salum amesema wamepokea maazimio hayo kwa mtazamo chanya na kwa idara ya elimu sekondari imeongezewa nguvu katika mikakati yake yakuimarisha elimu hasa kwenye eneo la kuongeza ufaulu wa kidato cha tano na sita kwa daraja la kwanza na pili pamoja na kuondoa ziro kwa kidato cha nne.
Hata hivyo amepongeza mkakati huo wa elimu kitaifa na kuwataka wasimamizi wa elimu kuzingatia maazimio yaliyotolewa ikiwa pamoja na kuwajibika moja kwa moja katika kuingia darasani kufundisha hiyo itasaidia kuinua hari kwa walimu shuleni kutoa huduma bora za elimu.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki milikiĀ©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa