Mbunge wa jimbo la Newala Mjini ambaye pia ni Waziri Ofisi ya Rais Kazi Maalum Mhe. George Mkuchika amewataka wazazi kuhakikisha wanaweka kipaumbele cha elimu kwa wandaa watoto wao na kuwapeleka shule.
Ameyaeleza hayo leo Tarehe 2/12/2021 katika ziara yake ya kuongea na wananchi kwa njia ya mikutano ya hadhara ambapo amesema serikali imejenga miundo mbinu ya kutosha katika sekta ya elimu ndani ya halmashauri ya Mji wa Newala kwa kuongeza madarasa na shule mpya hivyo huu ni wakati wa wananchi kunufaika.
Aidha amebainisha kuwa kwa shule za wasichana za kidato cha tano na sita Nangwanda pamoja na Kiuta zimekuwa shule kinara katika matokeo ya kitaifa mkoa wa Mtwara, hivyo ni wakati wa wananchi wa Newala kutumia fursa hiyo kuwawezesha na kuwahimiza watoto wao katika elimu kwa kuwa wanufaika wengi ni watoto waotoka mikoa ya mbali.
Mhe. Mkuchika ameeleza kuwa “sisi Newala wakati wenzetu wanapiga hatua mbalimbali za maendeleo, tulikua kama wahanga wa vita ya kudai uhuru ya ndugu zetu Mozambique, hivyo tulikua tunawaza sana kunusuru maisha yetu na serikali kwa kulijua hilo ndio maana sasa wametuletea shule mpya na kutuongezea madarasa”.
Hata hivyo Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa halmashauri ya Mji Newala kwasasa ipo kwenye ujenzi wa shule mpya ya mshingi ya miembe saba kata Luchingi, ujenzi wa shule ya sekondari Makondeko Kata ya Makote, shule mpya ya sekondari ukanda wa bonde la mto Ruvuma, kuanzisha shule za kidato cha tano na sita kwa wavulana shule ya Malocho kata ya Nanguruwe, na Nambunga kata ya Mnekachi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmshauri ya Mji Newala Mhe. Yusuph Kateule amnaye pia ni diwani wa Kata ya Nanguruwe amemshukuru mbunge huyo kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwatumikia wananchi wa halmashauri ya mji Newala, kwa kuwatafutia vyanzo mbalimbali vya kuwezeka utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuwaomba wananchi kumuunga mkono katika kipindi chake.
Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Mapindizi wilayani Newala Bi. Sophia Lipenye amewaambia wananchi kuwa chama kupitia ilani kimedhamiria kupeleka maendeleo kwa jamii, hivyo nguvu ya pamoja inahitajika kwa kuwa Newala imepata kiongozi hodari anayejali wananchi wake.
Ziara hii ya siku ya kwanza ametembelea na kuzungumza na wananchi wa kata za Nanguruwe, Tawala na Mkunya.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki miliki©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa