Bodi ya mfuko wa elimu halmashauri ya Mji Newala na kamati tendaji ya mfuko imefanya ziara ya kukagua miradi iyopewa fedha na mfuko huo zaidi ya shilingi milioni 155 na kuridhishwa na matumizi yake.
Mara baada ya ziara Mwenyekiti wa bodi hiyo Ndg. Jarome Linyembe amempongeza mkurugenzi wa halmashauri na watendaji wake kwa usimamizi nzuri wa matumizi fedha katika miradi ya elimu msingi na sekondari.
“Kwa kweli hali ya miradi inaonekana ni mizuri hata kwa kuiangalia hii inaonesha usimamizi wake ni nzuri tunampongeza sana mkurugenzi wa Mji Newala kwa kukubali kusikiliza maoni ya bodi na kusimamia utekelezaji wake.” ameeleza Linyembe.
Hata hivyo mwenyekiti huyo ametaka shughuli zote zinazotekelezwa na mfuko huo zifahamike kwa wananchi “fedha hizi ni michango ya wakulima na wananchi wa halmashauri hii kupitia mauzo ya mazao yao yanayouzwa kwa stakabadhi ghalani ikiwemo korosho, mbaazi na ufuta.”
Aidha Linyembe amesema lengo la mfuko huo ni kusaidia maendeleo ya elimu katika kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji, kutoa motisha pamoja na miundombinu ili kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha sekta ya elimu nchini.
Mkuu wa idara ya elimu sekondari Mwl. Diana Sonno amesema mfuko huo kwasasa umekuwa chachu ya kusaidia ukamilishaji wa madarasa, maabara pamoja na posho kwa walimu wa muda nah atua hiyo inapelekea kupunguza ukubwa wa changamoto zinazoikabili idara ya elimu kwa ujumla.
“Ndugu mwenyekiti wa bodi, tunashukuru sana uwepo wa mfuko huu yaani umekua msaada sana kwetu sisi watu wa elimu hasa idara yetu mumetupata fedha shilingi milioni 5 za kukamiliza madarsa 5, shilingi milioni 45 kukamilisha maabara 3, mumetoa shilingi milioni 50.15 kununulia viti 250 na meza 250 pamoja na madawati 250” Amefafanua.
Kwa upande wake mratibu wa mfuko huo Mwl. Innocent Kerenge amewashukuru wananchi kwa michango yao huku akifurahishwa na awamu ya kwanza ya utekelezaji kwa kupunguza changamoto ya kukosekana maabara katika shule za sekondari.
“kwa kweli nimefurahi sana mwaka jana hali ilikuwa mbaya hapa Sekondari ya Dr. Alex wakati wa mtihani wa taifa tulikuwa na maabara moja kwa masomo ya sayansi lakini kukamilika kwa hii nyingine itaondoa ile hali ya wasiwasi wakati wa mitihani kwamba itakuwaje?” Ameeleza Mwl. Kerenge.
Aidha pia miradi mingine iliyopewa fedha ni ujenzi wa chumba cha darasa shule ya msingi Mnanje shilingi milioni 20, madarasa mawili shule ya msingi Mpilipili shilingi milioni 40 pamoja na shilingi milioni 15 za kuchangia ujenzi wa nyumba ya mtumishi shule ya msingi Nambunga.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki miliki©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa