Halmashauri za Wilaya Newala Mkoani Mtwara, kupitia kamati zake za lishe, kwa pamoja zimetakiwa kutenga shilingi elfu moja kwa idadi ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano na kutekeleza kwa vitendo hatua za kuandaa bajeti endelevu, itakayo washirikisha wadau wengine wa lishe.
Rai hiyo imetolewa jana Alhamisi Novemba 22, 2018 na Mkuu wa Wilaya ya Newala Aziza Mangosongo, wakati anafungua Semina ya mpango wa uandaaji wa bajeti ya lishe 2019/2020 kwenye halmashauri, iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo ambapo amesema hatua hiyo ni muhimu katika kukabiliana na Utapiamlo.
Mkuu wa Wilaya ya Newala akiongea na wajumbe wa Mafunzo ya Mpango wa kuandaa bajeti ya lishe kenye halmashauri 2o19/2020 wilayani Newala
Mkuu wa wilaya alisema “Ndugu washiriki, lishe duni ni chanzo kikuu cha upungufu wa damu kwa wajawazito ambao huwaongezea uwezekano wa kupoteza maisha wakati au baada ya kujifungua, kwa upande wa watoto wachanga na wadogo, lishe bora katika siku elfu moja za mwanzo wa maisha yao, ni muhimu yaani tangu mimba kutungwa mpaka anapotiza miaka miwili ,ndio msingi thabiti wa ukuaji wa mwili na maendeleo yake ya kiakili katika kujifunza na uwezo mkubwa zaidi wa kujiingizia kipato.”
Kwa upande wake Mwezeshaji wa Masuala ya Mipango na Bajeti Kitaifa kutoka 0R-TAMISEMI, bwana Allan Bendera, amesema utekelezaji bajeti ya lishe ni mwitikio wa sera ya taifa kuhusu lishe hivyo ameziomba kamati kuwa na vikao kazi vya kujadili makubaliano sambamba na kupeleka elimu kwenye ngazi ya chini ya uongozi kuanzia mitaa, vijiji na kata.
Hata hivyo ameeleza kuwa halmashauri kutenga shilingi 1,000 kwenye bajeti ya lishe kwa kundi la watoto linatakiwa lipewe kipaumbele, “kwasasa masuala ya lishe yamepewa umuhimu pekee kwa kuangalia athari za kijamii na kiuchumi katika maeneo yetu tunayoishi, hivyo ni vema kujadili kwa kina ili kupata mipango mizuri, imara ambayo inaenda kuondoa matatizo ya Utapiamlo pamoja na Udumavu katika jamii.” alieleza Bendera.
Mwezeshaji wa Masuala ya Mipango na Bajeti Kitaifa kutoka 0R-TAMISEMI, bwana Allan Bendera.
Wenyeviti wa halmashauri hizo, Mheshimiwa Chitwanga Rashid Ndembo wa Wilaya na Mheshimiwa Abdul Katani Dudu, diwani wa Kata ya Julia aliyekaimu uwenyekiti halmashauri ya Mji wamesema watahakikisha mpango wa kutenga bajeti hiyo inafanikiwa japokuwa ipo changamoto ya vyanzo vya mapato.
Nao wajumbe wa semina hiyo wamesema, mafunzo hayo yamesaidia kutoa uelewa wa pamoja baina ya idara mbalimbali za halmashauri zinazohusika kuandaa bajeti hiyo, na kuahidi kuzingatia muongozo wake ili kufikia lengo kusudiwa serikali huku wakitoa pongezi kwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mtaa (OR-TAMISEMI) kwa kushirikiana na Taasisi ya Chakula na LisheTanzania na Wadau wa Maendeleo walioandaa Mafunzo hayo.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki miliki©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa