Wananchi wa Halmshauri ya Mji Newala wamepewa angalizo la kujikinga na baa la njaa kufuatia uhaba wa mvua uliojitokeza mwaka huu pamoja na mafuriko yaliyowapata wananchi wanaofanya shughuli za kilimo kwenye ukanda wa bonde la mto Ruvuma.
Rai hiyo imetolewa na wajumbe wa kamati ya fedha kwenye kikao chao kilichoketi Machi 20, 2023 ambapo Mwenyeketi wa Halamshauri ya Mji Newala Mhe. Yusuph Kateule kamewataka wananchi kuchukua tahadhari ya kuweka akiba ya chakula na kulima mazao yanayostahimili ukame.
“Kwanza sisi tunawapa pole wananchi waliopatwa na janga la mafuriko, Mungu azidi kuwatia nguvu na kuwaweka salama lakini kutokana na hali ya uchache wa mvua kwa mwaka huu na haya mafuriko yalitokea niwaombe wananchi tutunze chakula tulichonacho na kipindi hiki cha mvua kilichobaki tupande mazao yanayoweza kutunusuru au kupunguza makali njaa hali itakuwa mbaya zaidi”
Aidha Mhe. Kateule amewataka viongozi wa vijiji na kata watoa elimu kwa wananchi juu ya utunzaji chakula na kuanzisha utaratibu mpya wa kuuza mazao yao kwa kutumia vibali visivyo na malipo ili kuzuia uuzaji holela wa mazao pamoja na kudhibiti wizi ulioweza kujitokeza.
Naye Mheshimiwa Hamisi Namata diwani wa Kata ya Mtonya ameeleza kuwa hali ya chakula kwa wakazi wa Newala kwa sasa sio nzuri hivyo ameimba idara ya kilimo na taasisi zinazousika na utoaji wa taarifa ya hali ya chakula kuieleza serikali kuwa wananchi wa Newala wanahitaji msaada wa haraka wa chakula kwa kuwa mashambani hakuna mazao ya kutosha na sokoni bei zinapanda kwa kasi.
“Juzi sokoni kiloba cha unga cha kilo 25 kilikua shilingi elfu arobaini jana kilifika mpaka elfu hamsini na leo mpaka muda huu tunaoongea nimepita sokoni nimekuta ni shilingi elfu hamsini tatu na maduka yanayouza unga ni machache kwa kweli hali hii ni mbaya watu wanahitaji msaada” alisisita diwani Namata.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi ambae pia ni Afisa Kilimo wa Halmashauri hiyo Ndg. Calistus Komba amesema hatua za utoaji taarifa kupitia kitengo cha maafa zimeshachukuliwa na sasa wanakamilisha tathmini ili kufikisha mchanganuo wa mahitaji ili ufikishwe ofisi ya waziri mkuu ambayo ndiyo yenye dhamana na utatuzi wa majanga nchini.
Hata hivyo Komba amewashauri wakulima kutumia mbegu za muda mfupi na kupanda mazao yanayostahimili ukame ili kuendana na hali ya hewa ya mvua chache, ambapo maafisa ugani ngazi kata wapo tayari kutoa ushirikiano wa elimu kwa wakulima kuendana na hali halisi ya hewa hivyo popote kwenye changamoto wasisite kuwatumia kwa ajili ya kupata ushauri.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki miliki©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa