Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe, Gelasius Gaspar Byakanwa (Katikati) akisaini Mikataa ya Afua za Lishe na Katibu Tawala Mkoa Dr, Jilly Elibariki Maleko (Kushoto kwake) wakati Wakuu wa Wilaya wakisaini Mkataba wa Afua za Lishe.
Na, Lunanilo L. Ngela
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Gaspar Byakanwa ameongoza kikao cha Tathmini ya lishe mkoani Mtwara kilichofanyika mapema leo katika ukumbi wa mikutano wa Mkoa ikiwa ni utekelezaji wa Agizo la Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan. Katika kikao hicho wajumbe walipata nafasi ya kujadili kwa kina hali ya utekelezaji wa Afua za lishe kwa mwaka 2017/2018, Mikakati ya namna ya kuboresha Lishe kwa kipindi cha Septemba - Juni 2019 ikiwa ni pamoja na Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Mtwara kutia saini Mkataba wa utekelezaji wa Afua za Lishe.
Katika Kikao hicho Mkuu wa Mkoa na wajumbe walibainisha changamoto mbalimbali zinazozorotesha lishe mkoani Mtwara kuwa ni pamoja na matumizi ya chumvi isiyo na madini ya joto, wanawake wajawazito kutohudhuria kliniki, utapiamlo, kula kupita kiasi, kutofanya mazoezi ya viungo, upungufu wa damu na wanawake kujifungulia nyumbani.
Mkuu wa Mkoa amewagiza watendaji wote katika sekta ya Afya kuhakikisha wanatimiza wajibu wao ili kujenga jamii ya watu wenye afya njema inayoendana na kasi ya ujenzi wa Tanzania ya Viwanda. Amewaagiza pia Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanatekeleza kikamilifu makubaliano ya mkataba waliosaini wa Utekelezaji wa Afua za Lishe ikiwa ni pamoja na kuhakikisha tathmini inafanyika mara kwa mara ili kupima kiwango cha utekelezaji ambacho Wilaya imefikia.
Ofisi ya Habari Newala ilipata nafasi ya kuongea na Mhe. Aziza Mwongosongo Mkuu Mpya wa Wilaya ya Newala ambaye alipongeza uamuzi wa Mkoa katika kusimamia Lishe na aliahidi kutekeleza kikamilifu makubaliano yote ya Mkataba wa Afua za Lishe. Mheshimiwa Mwongosongo amekuwa akisisitiza wananchi wa Wilaya ya Newala kushiriki katika mazoezi ya viungo ili kujenga Afya bora inayoendana na kasi ya ujenzi wa Newala mpya.
Aidha, wajumbe wa kikao waliiomba Wilaya ya Nanyumbu kutoa uzoefu wa namna ilivyofanikiwa katika kuhamasisha jamii kutumia huduma za Afya jambo lililopongezwa sana na uongozi wa Mkoa pamoja na washiriki wengine wa kikao.
"Lishe bora, kwa maendeleo ya Mtwara"
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki milikiĀ©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa