Ili kuwa na ufanisi wa zoezi la utambuzi na chanjo ya Ng’ombe, Mbuzi na Kondoo, maafisa mifugo wa halamshauri ya Mji Newala wametakiwa kwenda kuwa elimisha wafugaji juu ya umuhimu wa zoezi hilo pamoja na ruzuku inayotolewa na serikali.
“Chanjo hii ya sasa ni lazima wachangie serikali imetoa ruzuku ya asilimia hamsini na mkulima atatoa asilimia hamsini kwa kila mfugo, napokea simu nyingi wakidai chanjo ni bure sio hivyo nendeni mkawaelimishe wajue”.
Rai hiyo imetolewa na afisa kilimo, mifugo na uvuvi wa halmashauri hiyo Ndg. Calistus Komba wakati anafungua mafunzo ya Mfumo wa Kitaifa wa Utambuzi na Afya ya Mifugo (UTAMBUZI) kwa maafisa hao.
Aidha Komba ameishukuru serikali kwa kuwajali wakulima na kufafanua kuwa mfugaji atachangia shilingi 500 kwa Ng’ombe mmoja na shilingi 300 kwa Mbuzi na Kondoo na kuwahimiza maafisa hao kwenda kufanya kazi yao kwa weledi ili kufanikisha lengo la serikali.
Kwa upande wake Daktari wa mifugo wa halmashauri hiyo Selestine Mgando amesema zoezi hilo ni la kitaifa ambapo kutakuwa utambuzi na kutoa chanjo kwa Ng’ombe kwa ajili ya kuzuia homa ya mapafu na chanjo ya Sotoka ya Mbuzi na Kondoo.
Dkt. Mgando ameeleza faida ya zoezi hilo “kuna faida kubwa sana kwa taifa na wafugaji wenyewe kwanza kabisa tunawakinga wanyama wetu, kudhibiti vifo vya wanyama, kudhibiti wizi na kuwezesha nchi kuingia katika masoko ya kimataifa kwa kukidhi vigezo”.
Hata hivyo Mgando amewasisitiza maafisa ugani kuzingatia mafunzo hayo na kuwaomba wafugaji kujitokeza kuchanja mifugo yao wapate faida mbalimbali ikiwa pamoja na kuongeza uzalishaji wenye tija utakaopelekea kuongeza kipato chao.
Akiwaelekeza washiriki wa mafunzo hayo afisa TEHAMA wa halmashauri Daud Matandiko serikali imeandaa programu maalum ya simu ya kukusanyia taarifa kupitia simu janja kwa ajili ya kufanikisha zoezi la utambuzi
“Na application hii inafanyakazi kwenye adroid peke yake, ni ka application nyepesi itakayo kuwezesha chukua taarifa za mkulima au mfugaji na taarifa za wanyama wake”. Amefafanua Matandiko
Hata hivyo katika zoezi hilo sambamba serikali kutoa ruzuku na chanjo lakini inatoa pete za utambuzi kwa Wanyama, malipo ya uendeshaji zoezi kwa wataalam pamoja na vishikwambi kwa kila afisa mifugo wa kata.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki miliki©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa