Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa ametoa wiki mbili kwa kamati ya ulinzi na usalama wilayani Newala kufanya uchunguzi wa kuyabaini makampuni binafsi yanayokopesha fedha kwa watumishi na kujua viwango vya riba vilivyopo pamoja na idadi ya watumishi waliokopa.
Mkuu wa Mkoa ameyasema hayo wakati anafunga mkutano wake wa kwanza wa kusikiliza kero za wananchi wilayani humo uliofanyika mwishoni mwa juma Mei 10 2019, katika viwanja vya mahakama ya mwanzo mjini Newala, ambapo amefafanua kuwa makampuni hayo yamekuwa yakikiuka taratibu nyingi za kibenki.
Byakanwa amewataja waalimu na jeshi la polisi kuwa ndio makundi vinara ya kuchukua mikopo kwenye makampuni hayo hivyo zoezi ka kuyabaini ni lazima lifanyike haraka kwa kuwa watumishi wengi wameweka viambata vyao muhimu kuwa dhamana kama kadi za benki na vitambulisho mbalimbali sambamba na kukatwa riba kubwa.
Katika hatua nyingine amewataka madiwani kuwaelimisha na kuwahamasisha wajasiriamali wadogo juu ya faida na umuhimu wa kuwa na vitambulisho vya ujasiriamali vilivyotolewa na Mhe. Rais Dkt. John Magufuli kwani ndio utetezi wao na jibu sahihi la kuepuka usumbufu wa tozo na ushuru wa biashara zao.
Aidha amewataka wajasiriamali wenyewe kutambua kuwa uwamuzi huo wa Mhe. Rais ni fursa kwao, hivyo wajitokeze kununua vitambulisho hivyo, ili visaidie kupata takwimu halisi ya idadi yao na aina ya biashara wanazofanya na kupelekea urahisi wa kuwatambua na hata kurahisisha taratibu za kibajeti pale zinapohitajika.
Hata hivyo kutokana na kujitokeza wananchi wengi wenye kero ya migogoro ya ardhi na kesi za usalama barabarani hasa kwa bodaboda, mkuu wa mkoa ameunda kamati ya ardhi ambayo imeipa mwezi mmoja kupitia changomoto zote za ardhi kisha kutoa ushauri wa kitaalamu na njia za kuipatia ufumbuzi, chini ya mwenyekiti wake afisa ardhi wa halmashauri ya wilaya ya Newala, afisa sheria wa mji Newala, wajumbe ni afisa kutoka ofisi ya DSO, afisa wa TAKUKURU, Maafisa watendaji wawili pamoja afisa Tarafa ya Newala.
Kamati nyingine ni kamati itakayosimamia kusikiliza na kutoa ushauri kwa mkuu wa mkoa kuhusu malalamiko ya madereva bodaboda na jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani ambayo imepewa wiki mbili kutekeleza jukumu lake, chini ya mwenyekiti wake, Mkuu wa TAKUKURU wajumbe ni afisa sheria wa halmashauri ya mji Newala, afisa kutoka ofisi ya DSO, afisa mmoja kutoka jeshi la Polisi na wawakilishi wa waendesha bodaboda wawili.
Kwa upande mwingine kutokana malalamiko ya baadhi ya wakulima wa korosho kutolipwa fedha zao mauzo katika msimu wa 2018/2019 amesema kumekuwa na kutofautiana kwa taarifa kati ya bodi ya mazao mchanganyiko ambayo inasema imewalipa wakulima na wakulima wanalalamika kutolipwa hivyo amechukua takwimu za wakulima hao ili kwenda kufanya ulinganifu na taarifa bodi kwa lengo la kubaini ukweli wa jambo hilo.
Aidha mkuu wa mkoa ametia shaka mwenendo wa kuanzishwa benki ya wananchi Newala, kufuatia malalamiko ya mwananchi mmoja aliyedai tangu mpango wa kuanzishwa kwa benki hiyo na ununuzi wa hisa mwaka 2012 mpaka sasa wananchi walionunua hisa hawajapewa mrejesho wowote kujua nini kinaendelea.
Byakanwa amesema wasiwasi unatokana na muda mrefu wa mchakato huo na wasimamizi kutofanya hata mkutano mmoja na wanahisa ili kuwapa ufafanuzi, hivyo amemtaka mwenyekiti wa bodi ya uanzishwaji benki hiyo kupeleka taarifa ya maandishi ofisini kwake na kwa pamoja wakutane na wataalamu wa benki kuu kujua kama upo uwezekanao wa kuanzishwa benki hiyo au kusitisha mchakato huo.
Awali akizungumza wakati anamkaribisha Mkuu wa Mkoa kuzungumza na wananchi Mkuu wa wilaya ya Newala Mhe. Aziza Mangosongo, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanya ziara wilayani hapa Aprili 03, 2019, ya kuweka jiwe la msingi ukarabati na upanuzi wa chuo cha ualimu Kitangali pamoja na kuongea na wananchi, ambapo mkuu wa wilaya ameahidi kuendelea kutekeleza yale yote aliyoagiza na anayoendelea kuagiza kwa lengo la kuwatumikia wanachi wa Newala na watanzania kwa ujumla.
Aidha amewataka wananchi wa Newala kwa ujumla kudumisha amani iliyopo na hata pale watakapoona kuna changamoto zimejitokeza vi vema wakazitafutia ufumbuzi kwa njia ya amani na haraka ili taifa na wilaya ipate ustawi wa maendeleo ya paomoja na mtu mmoja mmoja.
Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Newala Mussa Ramadhani Mwezi amesema hatua ya viongozi wa serikali walioteuliwa na Mhe. Rais kwenda kwa wananchi na kusikiliza kero zao ni utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi hivyo chama kitaendelea kusimamia makubalino yake ya kuwatumikia wananchi.
Akifungua mkutano huo Diwani wa Kata ya Luchingu Mhe. Bilali Othumani Bilali alizitaja kero za maji, umeme, ukamataji usio salama wa bodaboda na malipo ya korosho kuwa ni baadhi ya changamoto za wananchi wa wialaya ya Newala kero ambazo zilipatiwa majibu na Mkuu wa Mkoa.
Mkuu wa Mkoa Mtwara yupo kwenye ziara yake ya kikazi katika wilaya na halmashauri zote za mkoa huu kusikiliza kero mbalimbali za wananchi za binafsi, za kijamii na za kiutendaji.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki milikiĀ©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa