Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Aziza Mangosongo Jumamosi December 29,2018, amezindua rasmi zoezi la ugawaji wa vitambulisho vya wajasiriamali wadogo wilayani hapa, huku akitoa onyo kwa watakao toa taarifa za uongo kuwa watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa pamoja na kunyang’anywa kitambulisho.
Akizindua zoezi hilo, lililoitikiwa na wajasiriamali zaidi ya 1000 na 594 kati yao kupata vitambulisho hivyo wakati wa uzinduzi, Mhe. Mangosongo amesema wanaostahili kupata vitambulisho hivyo ni wale wenye sifa tu huku akimshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwaona wananchi wa hali ya chini walioamua kujitafutia kipato chao kwa njia halali, na kuamua kuwapunguzia adha ya tozo za ushuru kutoka kwa taasisi mbalimbali za fedha walizokuwa wanazilalamikia kwa muda mrefu.
Afisa wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wilayani Newala, bwana Yusuph Otieno, amesema wanaostahili kupata vitambulisho hivyo vilivyotolewa na Mhe. Rais ni wale wasio na namba ya utambulisho ya mlipa kodi ya biashara (TIN) na mauzo ghafi ya biashara zao yasiyozidi shilingi milioni 4 kwa mwaka au mauzo ya wastani wa shilingi elfu 12 kwa siku.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kuchukua vitambulisho hivyo, wamemshukuru Mhe. Rais kwa kuwajali na kuwathamini kwani awali walikuwa wanasumbuliwa sana na Maafisa kutoka idara za fedha za halmashauri, TRA na wakati mwingine Mgambo wanaotumwa kukusanya mapato ambao walikua hawaangalii hali ya kipato chao.
Aidha wamemuomba kuendelea kuwaangalia wananchi wa hali ya chini, huku wakiahidi kumuunga mkono kwenye jitihada zake za kuwatumikia watanzania katika kuwaletea maendeleo, uzinduzi huo umefanyila kwenye maeneo mawili tofauti wilayani hapa, ukumbi wa halmashauri ya wilaya Newala na Ofisi ya kata Kitangari.
Rais Dkt. Magufuli hivi karibuni alitangaza kuwapatia vitambulisho vyenye namba ya utambulisho wajasiriamali wote wadogo nchini, wenye mtaji wa mauzo ya biashara zao yasiyozidi milioni 4 kwa mwaka ambapo mjasiriamali huyo atatakiwa kulipia shilingi elfu 20 kwa mwaka mmoja.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki miliki©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa