Viongozi wa dini wa Halmashauri ya Mji Newala wametakiwa kuwa chachu ya mabadiliko ya kukomesha ukatili katika jamii na kusaidia malezi bora ya watoto ambao sasa wapo hatarini kutokana na kukithiri kwa matendo ya unyanyasaji.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya Newala Alhaj Rajabu Kundya wakati anafungua warsha ya ulinzi wa mtoto kwa viongozi wa dini, kamati ya ulinzi na usalama, wakuu wa shule na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa mtoto ya halmashauri ya Mji Newala.
Alhaj Kundya amesema kwa sasa kuna ongezeko kubwa la vitendo vya ukatili ambavyo vinatishia ukuaji wa watoto, hivyo malezi ya kiroho ndio njia muhimu itakayosaidia kubadilisha hali hiyo na kumfanya mtoto kuwa salama kimwili na kiakili.
Jamii yetu inavyobadilika inakwenda kwenye mabadiliko hasi maana yake tuanalegalega katikakutekeleza wajibu wetu na hivyo kuumba jamii ya watu ambao wamekata tama, watu wanaoishi kama wanyama na wasio namanufaa kwao wenyewe, kwa jamii yao na kwa taifa lao. Alisisitiza Kundya
Akiongea katika warsha hiyo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Newala Bi. Shamim Mwariko amesema viongozi wa dini ndio msingi wa ustawi wa jamii katika kuleta amani kuanzia ngazi ya familia mpaka Taifa kwa kuwa na viongozi na wananchi waadilifu.
Bi. Mwariko amefafanua kuwa kiongozi wa dini ana mamlaka ya kimungu inayosikilizwa na watu hivyo ni chombo muhimu kinachotegemewa katika kuimarisha mahusiano mema katika jamii kwa kuwawekea ulinzi watoto ili kujenga maadili yasiyoharibika na kuliendeleza taifa.
Akiongea kwa niaba ya vyombo vya ulinzi na usalama Mwakilishi wa Kamanda wa Polisi wilayani Newala OC-CID ASP Idd Omary amewataka viongozi wa dini kujiepusha na imani za itikali kali ambazo mara nyingi zinakuwa si za kizalendo na kubeba malengo ya uvunjifu wa amani.
Aidha ASP Omary ameeleza kuwa dini ndilo eneo hatarishi kwa amani ya Tanzania endapo viongozi wake hawatasimama imara katika kujenga umoja na mshikamano hivyo ni muhimu kuwa waangalifu katika kutumia majukwaa mbalimbali pamoja na kuhakiki mafundisho yanayotolewa kwa watoto kwenye makanisa na misikiti.
Mwenyekiti wa kamati ya amani na maridhiano ya wilaya ya Newala ambaye pia ni Shekhe Mkuu wa wilaya Yusufu Mikidadi amekiri kuwa jamii imeyumba kwenye ulinzi na malezi ya watoto kutokana na utandawazi pamoja na muda mwingi kutumika shuleni ambako hawapati malezi ya kiroho.
Mchungaji Atupakisye Ngonyani wa kanisa la EFATHA amesema pamoja na viongozi wa dini kubeba mzigo huo lakini serikali kupitia vyombo vyake nayo isimame katika nafasi yake ya kutofumbia macho matendo maovu ili jamii iwe salama kimwili na kiroho.
Warsha ya siku moja iliandaliwa na kitengo cha Ustawi wa Jamii halmashauri ya Mji Newala ililenga kujadili mada tatu ambazo ni Usalama ni jukumu la viongozi wa dini katika kuendeleza na kuimarisha amani, Ulinzi na usalama wa mtoto pamoja na Mabadiliko ya tabia Nchi.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki milikiĀ©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa