Viongozi wa kata na vijiji Halmshauri ya Mji Newala wametakiwa kusimamia ukusanyaji na upatikanaji wa chakula shuleni pamoja na kuhakikisha usalama wa chakula wanachopatiwa wanafunzi.
Agizo hilo limetolewa na mkuu wa wilaya Newala Mhe. Mwangi Rajabu Kundya Mei 08, 2023 wakati akizungumza na wajumbe wa kamati ya kikao cha kujadili utekelezaji wa afua za lishe ngazi ya Kata kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Mhe. Kundya ameeleza kuwa upatikanaji wa chakula kwa watoto shuleni kutaongeza umakini wa mtoto wakati wa kujifunza na kuimarisha afya ya akili hivyo viongozi wahamasishe wazazi kutambua umuhimu huo na kuchangia chakula bila shuruti
Aidha Mhe. Kundya ameelekeza waandaaji wa chakula lazima wazingatie usalama na afya za watumiaji kwa kuhifadhi na kuandaa chakula katika mazingira salama “laikini kingine ni hayo mazingira, mazingira ya usafi maana shuleni ndipo kilipo kitovu cha elimu, elimu ni pamoja na utaratibu wa chakula kwa nia ya kulinda afya zao”. Alieleza Mhe Kundya.
Katika kuhakikisha shule zinatoa huduma ya chakula kwa wanafunzi wawapo shuleni Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Yusuph Kateule amewaagiza maafisa watendaji wa kata kwenda kuzisimamia shule zote zenye maeneo ya wazi zianze kuzalisha chakula kwa kulima mazao mbalimbali ya chakula.
Aidha ameongeza kuwa hatua hiyo itasaidia kuanza kujenga mtazamo kwa wazazi kuona umuhimu wa kuchangia chakula na itapunguza kiasi cha wingi wa uchangiaji kwa kuwa shule zenyewe zitakua zimeonyesha njia.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bi. Shamimu Mwariko amesisitiza utaratibu wa utunzaji wa chakula uzingatiwe kwa kuhakikisha kinakaushwa na kuhifadhiwa sehemu salama itakayowezesha kukaa kwa muda mrefu bila kuharibika.
Hata hivyo amemtaka afisa lishe kuweka mpango wa kutembelea shule kujiridhisha juu ya hali ya ulaji wa watoto kwani wanaweza wakawa wanakula chakula kisicho na msaada wa kiafya na kimwili kutokana na mazingira mabovu ya utunzaji na uhifadhi, “Vyakula vinapoletwa shuleni vikaushwe katika kiwango kinachotakiwa viweke katika mifuko ya design ya kinganjaa au ya A to Z kwasababu ina uwezo wa kuweka hata miaka mitatu.” Alisisitiza
Kikao hicho cha robo ya 3 2022/2023 kiliketi kutathmini utekelezaji wa mkataba wa afua za lishe ngazi ya Kata kwa kata zote 16 za Halmashauri ya Mji Newala na katika kupitia taarifa zake ilionyesha baadhi ya shule hazitoi chakula na kuweka azimio la kuchangisha vyakula kwa wazazi.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki miliki©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa