Wakuu wa shule na walimu wa kidato cha sita Halmashauri ya Mji Newala wamepongezwa kwa jitihada zao za kuhakikisha wanafunzi wanafanya vizuri katika mtihani wao wa taifa mwaka 2025.
“Kwanza niwapongeze walimu wetu pamoja na wakuu wa shule kwa jitihada za dhati kabisa walizochukua katika kipindi hiki mpaka kupata matokeo haya, baadhi ya shule zilikuwa ndo zinaanza, baadhi ya walimu hawakuwa waozefu”.
Pongezi hizo zimetolewa na kaimu mkuu wa idara ya elimu sekondari Mwl. Innocent Kerenge kufuatia matokeo ya jumla waliyoyapata katika shule zake nne, mbili za wasichana zenye mchepuo wa sanaa na mbili za wavulana za mchepuo wa sayansi.
Kerenge amefafanua “Kati ya wanafunzi 408 waliofanya mtihani, waliopata daraja la kwanza ni 107 sawa 26%, waliopata Daraja la pili ni wanafunzi 262 sawa 64% ni wanafunzi 39 pekee waliopata daraja la tatu sawa na 10% hakuna daraja la nne wala sifuri katika shule zetu”.
Aidha Mwl. Kerenge amesema ni mpango wa halmashauri kuongeza ufaulu na kuondoa daraja la tatu, la nne na daraja sifuri huku akiishukuru serikali kwa kuwaongezea walimu wapya wataalam wa maabara, vifaa vya maabara pamoja na vitabu.
Kwa upande wake mwalimu wa somo la Historia katika shule ya sekondari ya wasichana Nangwanda Mwl. Happyness Haule amefurahishwa na matokeo hayo na kuwataka wanafunzi wanaotarajia kufanya mtihani ujao kuwa tayari kwa ajili ya mpango wa ufaulu wa juu zaidi.
Naye mwalimu wa fizikia na kemia katika shule sekondari ya wavulana Nambunga Mwl. Jonas Mgonya amekiri changamoto ya ugeni katika kufundisha kidato cha tano na sita kwani walimu wote shuleni hapo walikuwa wapya.
Hata hivyo Mwl. Mgonya amefurahishwa na serikali kumleta mtaalam maabara shuleni hapo “matokeo yaliyopita hatukua na mtaalamu wa maabara hivyo utatusaidia kuwainua hawa vijana kwa kufanya majaribio mengi ya vitendo yakutosha hivyo kuwezesha matokeo mazuri”.
Halmashauri ya Mji Newala ina shule nne za sekondari za kidato cha tano na sita shule sekondari ya wasichana Nangwanda, shule sekondari ya wasichana Kiuta, shule mbili mpya za wavulana zilizofanya mtihani kwa mara kwanza shule ya sekondari Nambunga pamoja na Malocho.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki miliki©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa