Wananchi wa halmashauri wa Mji Newala, wameishukuru serikali na mbunge wa jimbo la Newala mjini Mhe. George Huruma Mkuchika kwa kuwapatia gari la wagonjwa kwenye kituo cha Afya Mkunya.
Gari hilo limetolewa na Wizara ya Afya kwa ufadili wa GLOBAL FUND limekabidhiwa leo Alhamisi Mei 7, 2020 na Mkuu wa wilaya ya Newala Bi. Aziza Mangosongo ambae amefafanua kuwa serikali chini ya Rais Magufuli, inafanya kazi zake kwa kutekeleza ahadi zake ilizoahidi kwa vitendo kama zilivyo kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Aidha Mkuu wa wilaya amemshukuru Mbunge wa jimbo hilo Kapteni Mstahafu George Mkuchika kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwasemea wananewala mji kwenye kufanikisha kupata miradi ya maendeleo.
Akiongea baada ya kukabidhiwa gari hilo, mganga mkuu wa halmashauri hiyo Dkt. Athanas Emmanuel amesema gari hiyo ni mkombozi kwa idara ya afya kwani awali kulikuwa na changamoto ya uchakavu wa gari la wagonjwa, hivyo anaishukuru serikali kwa kutatua changamoto hiyo na ameahidi kulitunza gari hilo.
Kwa upande wake katibu wa siasa na uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Newala Ndg. Hamisi Namata, amesema CCM chini ya Dkt. Magufuliitaendelea kuwatumikia wananchi wake kwa kuwapelekea maendeleo kwa kutimiza ahadi zake, huku akitoa shukrani za Mhe. Rais na Mbunge kwa kutekeleza miradi mingi ya maendeleo katika jmbo hilo.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria makabidhiano hayo wameishukuru serikali kwa kusikia kilio chao cha muda mrefu huku wakiahidi kuiunga mkono kwa vitendo pamoja na kulitunza gari hilo.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki milikiĀ©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa