Wananchi wa Tarafa ya Mkunya Halmashauri ya Mji Newala mkoani Mtwara wameishukuru Serikali kwa kuwatatulia changamoto ya upatikanaji wa huduma za Afya kwa kuwajengea na kuwapatia wahudumu katika kituo cha afya Mkunya.
Wakiongea kwa nyakati tofauti hivi karibuni wakazi hao wamesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanyakazi kubwa ya kuwatumikia wananchi na wanamshukuru kwa kuwaboreshea huduma za afya.
Mzee Abdallah Mkamate (75) mkazi wa kijiji cha Pachoto amesema ni furaha kwa upande wake kituo hicho kuwa karibu kwa kuwa awali walikua wanapata shida kwenda mbali kufuata huduma katika hospitali za Newala, Ndanda, Nyangao , Luagala, Mkomaindo na Lindi.
Hata amempongeza Mhe. Dkt. Rais na mtangulizi wake Dkt. Magufuli kwa uongozi wao “sisi zamani tulikua tunakwenda huko kutibiwa haumjui mtu, haujui pakufikia na ukilazwa ni tatizo nani atakupa msaada au hata daktari hakujui kama hauna hela hauwezi hata kuomba, hapa unaweza hata ukajieleza kesho ukaleta pesa, kwahiyo uongozi wa sasa ni nzuri” Alieleza Mzee Mkamate.
Bi. Zena Mtave mkazi wa Mcholiwa Godauni amesema kwa sasa huduma za afya kwa wanawake na watoto zimeimarika tofauti na kipindi cha nyuma ambapo kulikuwa na uwezekano mkubwa wa wajawazito kupoteza maisha hasa pale inapojitokeza changamoto wakati wa kujifungua kutokana umbali wa kwenda kupata huduma za uhakika
‘Siku hizi kwakweli tunafurahi sisi wanawake tunapimwa, tunalazwa hapa hapa zamani tulikua tunataabika kwenda Newala hospitali ni mbali na kuna gharama za usafiri pikipiki yaani tulikua tunashindwa, naipongeza serikali, Mama Samia na wote wanao husika”. Alieleza Bi. Zena
Nae Bi. Aisha Athuman Mkazi wa kijiji cha matokeo amesema wanafurahia huduma wanazopata toka kwa wahudumu hasa huduma za watoto na upatikanaji wa dawa kutokana na utaratibu nzuri uliopo uliowekwa huku akiiomba serikali kuongeza dawa kwa kuwa zinazopatikana huwa zinaisha mapema.
Kwa upande wake Bw. Shaibu Abdallah mkazi wa kijiji cha Pachoto ameipongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa Afya za wananchi wa Tarafa ya Mkunya ambao mwanzo walifuata huduma hizo mbali na kuiomba kuwaboreshea katika kuongeza wataalamu na vifaa tiba.
Kituo Cha Afya Mkunya kimejengwa kwa fedha za Serikali kuu kwa gharama ya shilingi milioni 600 na kimekuwa mkombozi kwa wakazi wa tarafa hiyo na kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali kuu ya Newala.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki miliki©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa