Wataalam wa afya wanaosimamia huduma za mama mjamzito na watoto wachanga mkoani Mtwara wametakiwa kutambua lengo la Serikali la kuongeza vituo vya afya na majengo ya wazazi ni uhakika wa kuwa na uzazi salama.
Hayo yameelezwa Jumatano Julai 26, 2023 na Mkuu wa Wilaya ya Newala Alhaj. Mwangi Rajabu Kundya wakati anafungua kikao cha uchunguzi wa vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga mkoani Mtwara kilichofanyika kwenye ukumbi wa Chuo Cha Uuguzi Newala.
Alhaj. Kundya amesema serikali imeongeza vituo hivyo ikilenga kuokoa maisha ya mtoto mchanga pamoja na usalama wa wajawazito kwa kupata msaada wa kitaalam hasa pale inapojitokeza changamoto wakati wakujifungua.
Aidha amewataka wataalam hao kuonyesha thamani ya uwekezaji huo wa serikali kwa kuzingatia weledi wa kuwahudumia wananchi. “uwezekezaji huu utaleta tija endapo tuu.. watalam mtaboresha huduma za kitaalam kwa kuhakikisha mnatoa huduma kwa weledi, staha, kuwa na huruma na kuepusha lugha za kukatisha tama”. Alieleza Kundya.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara (RMO) Dkt. Hamad Nyembea, amesema mkoa umeamua kuandaa jukwaa hilo muhimu kufanya tathmini, kujipima pamoja na kuweka maazimio ya maboresho, kwa kuwa huduma za mama na mtoto mchanga ni kiashiria cha toaji huduma bora za afya kwa wananchi.
Dkt. Nyembea amesema kwa kuwa serikali imewajibika kwa vitendo kuboresha miundombinu kwenye sekta afya hivyo ni wajibu wao kupanga mikakati ya kupunguza hatari ya vifo na kutoa huduma bora hasa kwa wanawake wajawazito na watoto.
Hata hivyo ametaja malengo ya kikao hicho kuwa ni kupitia utekelezaji wa maazimio yaliyowekwa kwenye kikao kilichopita, utendaji kazi katika huduma za akina mama na watoto pamoja na kuangalia idadi ya vifo na sababu zakutokea vifo hivyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Newala Ndg. Geofrey Mnauye amewataka washiriki wa kikao hicho kukitendea haki kwa kuchangia mawazo sahihi yatakayowezesha kuleta matokeo yaliyokusudiwa ya kuisaidia jamii na taifa kwa ujumla.
Aidha ameongeza kuwa majadiliano yalenge kumaliza tatizo lililopo na kupunguza mijadala ya mara kwa mara ambayo haina matokeo. “Matarajio yangu katika rotation hii tunazokwenda mwisho wa siku RMO tutakuwa na ziro report maana yake vikao vitapungua kwa kuwa tatizo litakuwa limepungua”. Alifafanua Mkurugenzi huyo.
Kikao hicho cha uchunguzi wa vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga mkoani Mtwara ni cha siku tatu kuanzia Julai 26-28, 2023 kikiwahusisha wataalam wa halmashauri zote 9 za mkoa, na kinafanyika kila baada ya miezi mitatu kwa mzunguko wa kila halmashauri kuandaa kikao hicho.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki miliki©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa