Wadau wa lishe kwa kushirikiana na Maafisa watendaji wa Kata Halmashauri ya Mji Newala wametakiwa kutumia maarifa mbalimbali na mbinu bunifu za kuboresha hali ya lishe kwa jamii zitakazo fanikisha kufikia malengo ya serikali.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Mwangi Rajabu Kundya katika kikao cha tathmini ya utekelezaji wa afua za lishe ngazi ya kata robo ya nne 2022/2023 kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo siku ya Jumatano Julai 19, 2023.
Amesema watendaji wa kata kwa kushirikiana na wadau wanatakiwa kuweka mipango madhubuti ya kuhakikisha afua za lishe zinafikiwa kwa asilimia 100 ikiwa pamoja na kuazimisha siku yalishe, watoto wanapata chakula shuleni, kuzingatia makundi ya vyakula na mambo mengine yanayohusu lishe.
Mhe. Kundya amesema serikali inaendelea kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za afya kwa kujenga hospitali ambazo pia zinazotoa huduma ya Mama na Mtoto zinazopelekea kuwa na Taifa la watu imara wenye utimamu wa akili.
“Mama samia anafanya jitihada kubwa sana ya kuhakikisha anatujengea hospitali zinazotoa huduma za mama na mtoto naomba nendeni mkatafakari na kutumia akili ya ziada kwenye kufanikisha malengo yetu.” Alisisitiza Mkuu wa Wilaya
Kwa upande wake Mratibu wa lishe wa Halmashauri ya Mji Newala Ndg. Enos Kuzenza ameiomba jamii kushirikiana na viongozi ngazi ya kata na vijiji kuhakikisha wanachangia chakula shuleni ili watoto waweze kuwa na uwezo wa kupokea maarifa wanayofundishwa.
Kuzenza amesema jamii itakikwa ibadilike kwani bado takwimu zinaonesha wanafunzi wengi wahapati chakula shuleni “Kupitia kikao hiki tumeona takwimu zinazoonesha kwamba asilimia ndogo ya wanafunzi wanakula shuleni na tumeona shule zinazotoa chakula niwasihi wazazi na jamii kuwezesha chakula shuleni”. Amefafanua Kuzenza.
Katika kikao hicho Mkuu wa wilaya alitoa zawadi ya cheti cha ubora kwa kata iliyofanya vizuri katika kutekeleza afua kwa robo ya nne Kata ya Mkote ndio iliyoibuka mshindi ambapo diwani wa kata hiyo Mhe. Hamisi Kazibure alipokea hati hiyo.
Mhe. Kazibure amesema zawadi hiyo chachu ya kuendelea kufanya vizuri na wamejipanga kwenda kuongeza kutoa elimu ya unyonyeshaji na ulaji majumbani na shuleni kwani jamii inayo vyakula vyote changamoto waliyonayo hawana elimu ya mpangilio wa vyakula hivyo.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki miliki©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa