Watumishi wa serikali nchini wametakiwa kuwajibika ipasavyo katika nafasi zao, ili kurahisha kufikia malengo tarajiwa na kutengeneza uhusiano nzuri baina ya wananchi na serikali.
Wito huo umetolewa mwishoni mwa juma lililopita 09th March 2019, mjini Newala na Naibu Waziri Ofisi ya Rais –Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (OR-TAMISEMI) anaye shughulikia Elimu, Mhe. Mwita Waitara wakati anazungumza na watumishi wa serikali wa wilaya ya Newala kwenye ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Newala.
Mhe. Waitara alisema kila mmoja anapaswa kutambua nafasi aliyonayo ndio dhamana yake ya kiutumishi hivyo ni vema kuwajibika kwa kuzingatia taratibu, kanuni pamoja na matakwa ya kiutendaji ya ajira na mwajiri “hasa kwenye suala la muda, hakikisheni munatumia muda wa kazi wa serikali vizuri kwa kuwahudumia wananchi” alisisitiza.
Aidha Waitara alieleza watumishi watekeleze wajibu wao kwa kuangalia mahitaji ya wananchi na sio kufanyakazi kwa kuwaangalia viongozi hasa wanapokuwa kwenye ziara mbalimbali jambo ambalo halitavumiliwa “utakuta mtumishi haoni umuhimu wa kutatua kero fulani ya wananchi, mpaka asikie kuna kiongozi wa juu yake anakuja, wewe hautufai, tekeleza wajibu wako mambo mengine yaweke pembeni, kama unaitikadi nyingine za kisiasa hapa sio mahala pake, kwa kuwa upo kazini tekeleza kazi za serikali hakuna ugonvi”, aliongeza.
Hata hivyo aliyataja mambo matatu yanayoweza kusaidia utendaji bora kwa watumishi kuwa ni mahusiano mazuri kazini, uzalendo na mtumishi kujiamini katika nafasi yake na kuondokana na hofu kwani kufanya kazi bila kujiamini ni chanzo cha kuharibu utendaji wa kazi.
Akiongea awali wakati anamkaribisha Naibu Waziri huyo, Katibu tawala wa wilaya ya Newala (DAS) Bwana Daniel Zenda kwa niaba ya Mkuu wa wilaya, aliwataka watumishi wa serikali wilayani hapa kufanyakazi kwa bidii na kuzingatia uadilifu kazini.
Naibu Waziri huyo, yupo mkoani Mtwara tangu 06th March 2019 kwenye ziara yake ya kikazi ya kuzitembelea halmashauri zote tisa (9) za mkoa huu, kukagua miradi ya elimu na kuongea na watumishi wa serikali.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki miliki©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa