Mbunge wa Jimbo la Newala Mhe. George Huruma Mkuchika ambae pia ni Waziri Ofisi ya Rais Kazi Maalum amewataka madiwani na wadau wengine wa elimu kuhamasisha elimu katika maeneo yao kwani wao ndio daraja kuu la kuunganisha kati ya jamii na walimu.
Ameyasema hayo Machi 31, 2023 wakati akiongea na wadau wa elimu na wazazi waliohudhuria kwenye hafla ya kilele cha wiki ya elimu iliyofanyika kwenye ukumbi wa halmshauri ya mji Newala ambapo amewasisitiza wadau wa elimu kuzingatia lishe kwa kuhakikisha chakula kinapatikana shuleni ili kuwawezesha wanafunzi kusoma kwa utulivu.
Mhe. Mkuchika amesema ni lazima kuwa na nguvu ya pamoja kwa Viongozi na wazazi waungane kuhakikisha chakula cha kutosha kinapatikana shuleni na kwa kufanya hivyo mahudhurio ya wanafunzi yatakuwa mazuri hali ambayo moja kwa moja ujifunzaji utaongezeka na utoro utapungua.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Mwangi Rajabu Kundya amewapongeza walimu kwa jitihada wanazozifanya katika ufundishaji shuleni pamoja na jukumu kubwa la malezi walionalo watoto wawapo shuleni na kuwasisitiza kuendelea kufanya hivyo kwa kuwa hiyo ndio taaluma yao.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bi. Shamim Mwariko amewataka wadau wa elimu kwa kushirikiana na wazazi kuimarisha malezi ya watoto kimaadili ambayo kwasasa yanaonekana kushuka kutokana ulimwengu unavyokwenda jambo linalosababisha na masuala ya elimu kuporomoka hivyo umakini mkubwa unahitajika.
"Kila mmoja kwa nafasi yake anatakiwa kuwajibika katika kuwalinda watoto kutokana na kuporomoka kwa maadili katika jamii yetu. Kwa maana hiyo popote alipo mtoto, mzazi au mdau wa elimu bila kujali mtoto ni wako au sio wako lazima kumwangalia kwa jicho la tatu kwani chachu ya elimu inatokana na sisi walezi kuonesha nia ya watoto wetu kupata elimu" Amesema mkurugenzi huyo
Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri Mwl. Athman salum, amesema serikali kwa upande wake imeshaweka mazingira rafiki ya miundo mbinu na licha ya upungufu wa walimu wanafunzi wamekua wakifanya vizuri hivyo walimu wanastahili pongezi kwa jitihata zao kwa kutoa elimu kutokana na nguvukazi iliyopo.
Kwa upande wao baadhi ya wadau waliohuduria hafla hiyo Mwl. Hadija Mpunga Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingim Karume na Mwl. Richard Mkambala shule ya Sekondari George Mkuchika wameipongeza Halmashauri na Wilaya kwa ujumla kwa hatua waliyoichukua ya kuwaongezea hamasa katika ufundishaji pamoja na wanafunzi katika kujifunza kwa kuwa ushindaji wa ufundishaji na ufaulu utaongezeka.
Maadhimisho ya wiki la elimu hufanyika kila mwaka yakiwa na lengo la kutathmini maendeleo ya elimu kwa ngazi ya halmashauri, mkoa na taifa, ambapo Serikali inatoa hamasa kwa wadau kuchangia na kuwekeza katika elimu, kujadili na kuweka mikakati wezeshi ya kuboresha miundombinu kwa maendeleo ya elimu pamoja na kutoa zawadi mbalimbali kwa walimu na wanafunzi waliofanya vizuri.
Newala-Mtwara
Anwani ya Posta: P.O.BOX 39
Simu: (+255) 023 2935398
Mobile: PS (0684439199)
Barua pepe: info@newalatc.go.tz
Haki milikiĀ©2017 NTC. Masharti yote yanazingatiwa